KITENDO DR Congo kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaweza kuwa neema kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu a Bara hasa Simba na Yanga, kwani mastaa wanaotoka huko kama Yannick Bangala, Henock Baka Inonga na wenzao wamelainishiwa gharama ishu za vibali vyao.
Klabu hizo zitaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingegharamia vibali vya wachezaji hao kama ilivyokuwa awali kabla nchi hiyo haijajiunga na jumuiya hiyo.
Katika Ligi Kuu Bara klabu za Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar na Geita Gold zina mastaa kutoka DR Congo akiwamo Fiston Mayele, Djuma Shaban, Yannick Bangala, Chico Ushindi, Heritier Makambo na Jesus Moloko waliopo Yanga, huku Simba ikiwa na Chris Mugalu na Henock Inonga wakati Azam in Idris Mbombo. Mtibwa inaye Deo Kanda na Geita yupo Erick Yema ilhali Namungo ina David Molinga, huku katika Ligi ya Championship timu za DTB na Kitayosce zikiwa na mastaa kutoka nchi hiyo.
Kwa sasa zitakuwa na unafuu katika kugharamia malipo ya viza za kuingia nchini na vibali vya kuishi kwani watalipa kiasi kidogo kutokana na unafuu utokanao na kuwa wanachama wa EAC kama ilivyo kwa wachezaji kutoka nchi nyingine wanachama.
Awali wachezaji kutoka DR Congo kila mmoja alilazimika kulipiwa viza ya kuingia nchini Dola 50 (Sh116,000), lakini siku za usoni hakutakuwa na malipo ya viza kwa vile raia kutoka EAC hawalipii gharama hizo wanapotoka nchi moja kwenda nyingine. Unafuu mkubwa zaidi utakuwa katika za vibali vya makazi anbapo awali mchezaji mmoja kutoka DR Congo alilazimika kulipiwa Dola 2050 (Sh4.7 milioni) kibali cha miaka miwili.
Kwa sasa klabu ambazo zitasajili wachezaji kutoka DR Congo kila moja itatakiwa kulipa Dola 550 (Sh 1.3 milioni) kwa kila mchezaji kwa kibali cha makazi ambacho ni tozo ya kibali kwa raia kutoka nchi za EAC. Uamuzi huo huenda ukawa na faida zaidi kwa Simba na Yanga kwani ndizo zinasajili idadi kubwa ya wachezaji kutoka DR Congo.
Kwa nyota wa Simba na Yanga pekee ambao wapo wanane maana yake timu hizo kwa pamoja zimelipa kiasi cha Dola 16,400 (Sh38 milioni) kwa vibali vya makazi, lakini kama ingekuwa baada ya kujiunga na EAC zingelipa Dola 4,400 (Sh10 milioni).
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle aliliambia gazeti hili kwamba upo unafuu kwa nchi za EAC katika baadhi ya nyanja kulinganisha na zisizo wanachama.
“Kuna unafuu ambao utapatikana katika hilo kwa sababu mwanzo walikuwa wanalipa viza, lakini kwetu Uhamiaji tukiletewa hiyo document (nyaraka ya kujiunga EAC kwa DR Congo) ndio tutaangalia serikali imeondoa vitu gani ambavyo huwa wanakaa na kukubaliana,” alisema.
Akizungumzia DR Congo kujiunga na EAC, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wameupokea kwa mikono miwili na wamefurahia.
“Ukiondoa unafuu katika hizo tozo za vibali, lakini pia unakuza utangamano na ushirikiano baina ya DR Congo na Tanzania na sasa watakuwa ni kama ndugu zetu. Kuna maeneo mengi ambayo kama nchi tutanufaika nayo kwa mfano sasa itakuwa ni rahisi kuwepo kwa ushirikiano baina ya klabu za Tanzania na za DR Congo na pia wizara,” alisema.
Wakili na mdau wa soka, Phillip Ilungu alisema kuwa uamuzi huo utakuwa na tija kwa soka la Tanzania.
“Itasaidia sana kupata wakufunzi wabobezi kutoka DR Congo na kutakuwa na wepesi wa vibali vya kazi kupitia mgongo wa Jumuiya,” alisema.