Meneja wa Habari na Mawasialino wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally amesema hakuna wa kuizuia klabu hiyo kutinga hatua ya Robo ya Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.
Simba SC itakua mwenyeji wa USGN ya Niger Jumapili (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho, huku ikihitaji ushindi ili kujihakikishia kucheza Robo Fainali.
Ahmed ametoa kauli hiyo ya kujiamini alipozungumza na Mashabiki na Wanachama wa Simba SC makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi Jijini Dar es salaam Mapema jana Ijumaa (April Mosi).
Ahmed amesema maandalizi ya kikosi chao yapo vizuri na wanatarajia kuona kikipambana ipasavyo dhidi ya USGN na kufuzu Robo Fainali.
“Jumapili ndio jambo kubwa, Jumapili tunakwenda kuamua hatma yetu ya kucheza Robo Fainali, hakuna wa kutuzuia, wakiwa wamelala watatukuta tupo Robo Fainali.”
“Muda ni Saa Nne Kamili Usiku, niwatoe hofu wanasimba, hiyo ndio mida ya wakubwa na Mwanasimba hachagui muda wa kwenda kuiangalia timu yake, hata wangetupiangia Saa Moja Asubuhi, tungeamka tukaenda uwanjani, huo ni Usiku wa Wakubwa.”
“Mambo makubwa hufanyika usiku, hata dua za Usiku Mungu huzipokea bila kipingamizi, wanasimba wenzangu cha kufanya ni kimoja tu, nunueni tiketi na mfike Uwanjani kuishangilia timu yenu.” amesema Ahmed Ally
Katika Msimamo wa ‘Kundi D’ Simba SC ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiongoza kwa kufikisha alama 09.
USGN itakayocheza dhidi ya Simba SC, ipo nafasi ya nne kwa kufikisha alama 05, hivyo itahitaji kushinda huku ikiiombea mabaya RS Berkane ipoteza dhidi ya ASEC Mimosas siku hiyo ya Jumapili (April 03).