RELIANT Lusajo wa Namungo ana mabao 10 kama Fiston Mayele wa Yanga katika orodha ya Wafungaji wa Ligi Kuu Bara. Hapa nyuma yao kuna chuma kinaitwa George Mpole wa Geita ameshatupia nane.
Wanaofuata kila mmoja anaonekana kuwa moto na mabao yake sita mkononi ni Meddie Kagere(Simba), Saido Ntibazonkiza(Yanga), Vitalis Mayanga(Polisi). Lakini Kocha wa Berkane ya Morocco, Florent Ibenge amesisitiza kwamba msimu huu ni wa Mayele tu.
Amedai kwa rekodi za wachezaji hao wengine zilivyo, haoni mwenye moto wa kumzuia Mayele kubeba kiatu msimu huu.
Ibenge amefichua pia kuwa; “Kitu bora kwake anafanya kazi katika klabu ambayo ina mashabiki wengi na wanaowapenda wachezaji wao, wakati Yanga wanamtaka nilimwambia ni bora aende Tanzania kuliko kwenda Uarabuni angeweza kupotea nafikiri nilimshauri vizuri.”
Ibenge alisema mabao 10 aliyofunga Mayele hadi sasa ni kama jamaa anaanza kuchanganya na kama ataendelea kucheza mechi zote zilizosalia anaweza kufunga hata mabao 20 mwisho wa msimu.”
Kocha huyo ambaye hajawahi kuishinda Simba tangu aanze kuja nchini akipoteza mara tatu alisema kitu bora kwa Mayele ni mshambuliaji asiyesubiri kutengenezewa nafasi na huwa anahusika kutengeneza mashambulizi.
“Kama akiendelea kucheza hayo mabao 10 ni machache atafunga hata mabao 20 au zaidi namjua vizuri hizo mechi 12 zinamtosha kabisa kufikia malengo hayo,” alisema Ibenge atakayeiongoza Berkane kucheza nyumbani dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast katika mchezo wa kukamilisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
“Unajua uzuri wa Mayele ni mshambuliaji aliyebarikiwa kuwa na vitu vingi, washambuliaji wengi huwa wanasubiri kutengenezewa ila Mayele anashiriki kutengeneza mashambulizi.
“Nafikiri mnamuona hapo anavyopambana na mabeki anavyokimbia ana kasi sana lakini analijua lango, hiki ni kitu cha kipekee nilivyokuja hapo nilimwambia nafurahi kuona anafanya vizuri na anatakiwa kuongeza nguvu zaidi.”
Aidha Ibenge aliongeza, kitu ambacho kimefurahisha zaidi ni jinsi Mayele alivyojitengezea umaarufu kupitia mtindo wake wa kushangilia ambao umekuwa gumzo nchini.