SHABIKI mmoja wa klabu wa Asante Kotoko, Martin Kyei (32) amewaacha watu hoi baada ya kuvua nguo zote na kubaki uchi kisha kuingia uwanjani kushangilia baada ya Timu yake hiyo kuwafunga mahasimu wao, Accra Hearts of Oak ‘The Phobians’ kwa bao 1-0, juzi Jumapili, Aprili 10, 2022.
Kotoko ambao pia wanafahamika kama Porcupine Warriors waliibuka na ushindi huo katika Dimba la Baba Yara Sports Stadium mjini Kumasi nchini Ghana kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Franck Mbella Etouga baada ya kiungo wao Fabio Gama raia wa Brazil kuchezewa faulo dakika za lala salama, bao lililoibua hisia za furaha kwa shabiki huyo na kufanya maamuzi hayo magumu.
Taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari nchini humo zinadai kuwa, shangwe la jamaa huyo lilichagizwa na kile kinachosemwa kuwa alikuwa amebet, hivyo kwa ushindi huo tayari akawa amepiga mkwanja wa kutosha.
Lakini akihojiwa na kituo cha Asempa FM, Martin alikana kubet huku akisema kuwa hajawahi kubet.
“Sijui jinsi ya kubet, sijawahi kubet mechi yoyote, wala sikuwa nimekunywa kilevi chochote, mimi ni shabiki wa Kotoko, nilikuwa na furaha sana baada ya ushindi ule.
“Ninaomba kutumia nafasi hii kuomba radhi kwa mtu yoyote niliyemuudhi kutokana na kitendo changu hicho. Sitarudia tena maishani mwangu.
Katika video iliyosambaa mitandaoni inamuonyesha Martin akipanda juu ya uzio kutoka upande wa mashabiki na kushuka ndani ya uwanja akiwa uchi wa mnyama na kushikilia skafu yenye nembo ya Asante Kotoko jambo ambalo liliwaibua walinzi wa uwanja huo na kuanza kumfukuza kisha kumkamata na kumtoa nje.
Kwa sasa, Kotoko anaongoza Ligi Kuu nchini Gahana akiwa na pointi 52 mbele ya Bechen United wenye pointi 44, wakati Heart of Oak wakishika nafasi ya 6 na pointi 36.