Uongozi wa Simba SC umesema hauna mpango wa kuomba kusogezwa mbele kwa mchezo Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, uliopangwa kuchezwa April 30.
Young Africans watakuwa wenyeji wa Simba SC katika mchezo huo, utakaounguruma jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Baada ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, Simba SC itakuwa na siku sita za kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Mulamu Nghambi amesema klabu yao haina mpango huo, zaidi ya kuamini muda wa kujiandaa kukabili Young Africans utatosha, licha ya kukabiliwa na mchezo wa Mkondo wa Pili dhidi ya Orlando Pirates.
“Siku sita zinatutosha sana kuifanyia Young Africans maandalizi na tukaifunga, wala sio tatizo kwetu, japo ni kweli kwa upande wa nje timu itakuwa na ratiba ya mechi ngumu, lakini sio tatizo kwa klabu yetu.” amesema Mulamu
Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 41, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 51, huku kila mmoja akicheza michezo 19.