Mashabiki wa Yanga waliokuwa na hamu ya kuona kifaa kipya kutoka Rwanda kikitua Jangwani, wakae kwa kutulia baada ya Waarabu kutia mkono dili la kiungo Bigirimana Obed aliyefuatwa Kigali na mabosi wa klabu hiyo inayoongoza Ligi Kuu.
Inaelezwa mara baada ya Yanga, kuonesha nia ya kutaka saini ya kiungo huyo fundi wa mpira raia wa Burundi anayekipiga Kiyovu Sports ya Rwanda, fasta waarabu wa Tunisia nao wameingia mawindoni kuitaka saini ya nyota huyo lakini Yanga inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili mapema tu.
Taarifa zinadai kuwa juzi kuanzia saa 5:00 asubuhi za Rwanda ambazo ni sawa na saa 6:00 mchana za Tanzania, Injinia Hersi Said na Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze walikutana na Bigirimana katika hoteli ya Marriott mjini Kigali kuzungumza mambo ya kimkataba na kubaini kuwa waarabu wa Tunisia (Esperance Sportive de Tunis)tayari wametia miguu kwenye dili hilo hivyo wanatakiwa kufanya fasta kuhakikisha anatua Jangwani la sivyo watamkosa.
Hersi na Kaze walidokezwa ishu hiyo ya waarabu kumtaka Bigirimana na Rais wa Kiyovu, Mvukiyehe Juvenary aliyeambatana na nyota huyo sambamba na kocha Mkuu wa Kiyovu, Mrundi Harigingo Francis na meneja wa Bigirimana aliyejulikana kwa jina moja la Aruno kwenye kikao hicho.
Katika kikao hicho kilichodumu kwa muda kama wa nusu saa hivi, pande zote mbili zilikuwa zinaongea kuhusu dili hilo kwa mapana ambapo baadae walifika muafaka kuwa Yanga inatakiwa kuilipa Kiyovu Dola 90,000 (zaidi ya Sh 200 milioni).
Rais wa Kiyovu, Mvukiyehe alisema mazungumzo yapo kwenye hatua nzuri, ila kwa sasa hawatamuachia Bigirimana hadi msimu uishe na huenda akatua Yanga, Esperance au akatimkia zake Ubelgiji kwenye moja ya timu za Ligi Daraja la Kwanza ambao hakuitaja.
“Yanga tumeongea nao ila hatujafika mwisho. Bigirimana ni mchezaji mzuri na hadi sasa tuna ofa kutoka Esperance na nyingine kutoka Ubelgiji, ila zote hatujafikia makubaliano ya mwisho licha ya kwamba kuna uwezekano akaondoka mwisho wa msimu kwenda kwenye moja ya timu hizo au nyingine,” alisema Mvukiyehe.
Inaelezwa kuwa Yanga ina nafasi kubwa ya kumpata Bigirimana kutokana na mchezaji huyo kutaka zaidi kuja kucheza Tanzania na kuikacha Ofa ya Esperance ambako atahitajika kwenda kufanya majaribio kabla ya kusajiliwa.
“Bigirimana mwenyewe anataka kuja Yanga kuliko huko kwingine, ila ni lazima kama Yanga wamelizane na na Kiyovu na kwa maslahi yake binafsi kuhusu mkataba na malipo ni vitu ambavyo wataelewana kwani ndoto yake ni kucheza michuano mikubwa Afrika msimu ujao.” kilieleza chanzo chetu kilicho karibu zaidi na kiungo huyo ambacho hakikutaka jina lake kutajwa.
Baada ya kikao hicho kizito Hersi na Kaze walienda kujiandaa kabla ya kwenda Uwanja wa Ndege na saa 8 mchana kuianza safari ya kurudi Tanzania.
Bigirimana ni mzaliwa wa Uvira, DR Congo lakini aliyekulia na kupata uraia wa Burundi hadi sasa amefunga mabao tisa katika Ligi Kuu ya Rwanda na kutoa asisti tano na ni kati ya wachezaji tegemeo wa timu Kiyovu.