SIO poa. Mtu mmoja asiyefahamika amemwambia beki na nahodha wa Manchester United, Harry Maguire watafyatua mabomu matatu yaliyotegwa nyumbani kwake kama ataendelea kugoma kuchukua uamuzi wa kuachana na klabu hiyo ya Old Trafford.
Maguire kwa sasa anaishi kwa mchezaji mwenzake huku familia yake ikipelekwa kwenye makazi salama kufuatia barua pepe ya vitisho vikali iliyotumwa kwa wakala wa mchezaji huyo. Mtu huyo asiyefahamika amempa Maguire saa 72 za kuondoka Man United la sivyo watafyua mabomu matatu yaliyotegeshwa nyumbani kwake.
Barua pepe yenye ujumbe huo wa kitisho imetumwa kwa wakala wa Maguire, ukiwa na msisitizo kwamba mabomu yaliyotegwa nyumbani kwa beki huyo yatafyatuliwa kama atakiuka masharti ya kuondoka ndani ya muda huo uliopangwa.
Maguire, 29, alikuwa kwenye uwanja wa mazoezi Carrington wakati meseji hiyo ya vitisho inatumwa Jumatano iliyopita, siku moja baada ya Man United kudhalilishwa na Liverpool kwa kichapo cha mabao 4-0 uwanjani Anfield kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Alikimbiza gari haraka kurudi nyumbani kwa mchumba wake, mrembo Fern Hawkins, 27, wanaoishi na watoto wao wawili wa kike. Polisi na mbwa wa kunusa mabomu walipelekwa kwenye jumba hilo analoishi Maguire na familia yake lenye thamani ya Pauni 4 milioni huko Cheshire, lakini hawakuona kitu.
Na sasa mrembo Fern na watoto wao wa kike, Lillie Saint, 2, na Piper Rose atakayetimiza mwaka mmoja mwezi ujao wamepelekwa kwenye makazi salama. Maguire anaishi kwa mchezaji mwenzake kwa sasa. Polisi walikwenda tena nyumbani kwa Maguire siku ya Alhamisi kutafuta mabomu. Hawakupata kitu.
Chanzo cha habari hiyo kilifichua: “Hii kitu imechukuliwa siriazi sana. Harry na wachezaji wenzake mara kwa mara wamekuwa wakipokea vitisho vya kuuawa kwenye mitandao ya kijamii, lakini ya sasa imekuwa tofauti. Barua pepe ilisema kuna mabomu matatu yametegwa nyumbani.
“Amepewa saa 72 za kuondoka Man United mabomu hayo yatafyatuliwa. Inatisha sana.”
Chanzo hicho kiliendelea: “Fern alitetemeka sana. Haoni kama kuna usalama tena. Amechoshwa na manyanyaso anayopata Harry. Amesema imetosha.”
Barua pepe hiyo imeripotiwa kutoka kwa mtu aliyejitambulishwa kwa jina la ‘cowardly fan’.
Man United imekuwa kwenye kiwango kibovu huku beki huyo wa kati anayelipwa Pauni 190,000 kwa wiki alizomewa uwanjani na amekuwa akipokea kejeli nyingi kwenye ukurasa wake wa Instagram kutokana na kiwango cha hovyo anachoonyesha uwanjani.
Kuna baadhi ya meseji zimekuwa zikijirudia kwenye mtandao wa kijamii, zinazosema: “Ondoka kwenye klabu yangu.” Meseji moja ilisomeka hivi: “Bao jingine la kujifunga shukrani shetani mwenyewe.”
Kulikuwa na wasiwasi kama Maguire angepangwa katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal huko Emirates jana Jumamosi. Na sasa nyumbani kwake kumewekwa kamera mpya za CCTV na walinzi zaidi wanaofanya kazi kwa saa 24. Chanzo hicho kiliongeza: “Harry hapendi kuishi haya maisha, lakini kwa kipindi hiki hana chaguo. Hawezi kuiacha familia yake iendelee kupata vitisho.”