Kocha wa KMC, Thierry Hitimana hafurahishwi na mwenendo wa timu hiyo hii ni baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Geita Gold.
Akizungumza Hitimana alisema changamoto pekee imekuwa kwenye safu yake ya ushambuliaji na ulinzi hali ambayo inaifanya kutokuwa na uwiano sawa wa mabao ya kufunga na kufungwa kwa msimu huu.
“Ushindani umekuwa mkubwa na kila timu inapokuwa nyumbani imejipanga vizuri, pointi hatujapishana sana hivyo yeyote anaweza kufikia mahali fulani kama atapambana zaidi kutokana na malengo yake,” alisema na kuongeza;
“Kutokufunga kwa washambuliaji wangu ni jambo la kawaida tu kwa sababu hali kama hiyo humtokea yeyote na ninachoamini siku ambayo wataanza kupata bao basi ile morali yao ya kujiamini itarejea tena upya.”
Katika michezo minne iliyopita ya timu hiyo safu yake ya ushambuliaji haijapata bao lolote huku kwenye michezo 21 iliyocheza safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 20 huku nyavu zake zikitikiswa mara 23. Mbali na hilo ila KMC haijaonja ladha ya ushindi kwenye michezo mitano iliyopita kwani mara ya mwisho kushinda ilikuwa Februari 26, ilipoifunga Polisi Tanzania mabao 3-0. Inashika nafasi ya tisa na pointi 24.