Home Habari za michezo MWAMUZI ‘MNOKO’ AKABIDHIWA SIMBA vs USGN…KANOUTE NA ONYANGO WAONYWA…PAWASA ‘ATIA CHUMVI’..

MWAMUZI ‘MNOKO’ AKABIDHIWA SIMBA vs USGN…KANOUTE NA ONYANGO WAONYWA…PAWASA ‘ATIA CHUMVI’..


NYOTA wa Simba akiwamo Joash Onyango na Sadio Kanoute wametakiwa kuwa makini katika pambano lao la mwisho la Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN, kwani mechi hiyo imepewa mwamuzi mwenye rekodi za kugawa kadi.

Simba na USGN zinavaana Jumapili ya wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ili kuamua hatma ya kufuzu robo fainali, lakini habari ya kushtua ni kwamba pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi Helder Martins.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ni kwamba Helder Martins kutoka Angola ndiye aliyeteuliwa kulichezesha pambano hilo litakaloanza saa NNE Usiku na sifa yake kuu ni mwepesi kutoa kadi kwa wachezaji, jambo ambalo mastaa wa Simba wanapaswa kujihadhari ili wasitibue mipango Msimbazi.

Kwa sasa rekodi zinaonyesha Onyango na Kanoute ndio wachezaji wa Simba wenye kadi mbili za njano kila mmoja, hivyo kutakiwa kuwa makini wasikumbane na kadi nyingine zinazoweza kutibua timu ikitinga robo fainali.

Nyota hao wameonyesha kadi mbili kila mmoja kwenye michezo mitano iliyopita, hivyo kitendo cha kuonyesha nyingine (moja kila mmoja), kitawafanya kukosa mchezo mmoja ujao hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo ya kimataifa ngazi ya klabu ambayo yanasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Rekodi za Helder inaonyesha kwenye michezo 10 ya mwisho kuhusika kimataifa, ni mitano aliyochezesha huku mingine akiwa kama mwamuzi wa akiba.

Katika michezo hiyo mitano aliyochezesha, ametoa jumla ya kadi za njano 16 na nyekundu mbili kwa maana kwamba, Muangola huyo ana wastani wa kutoa zaidi ya kadi tatu kwa kila mchezo.

Mchezo wake wa mwisho kucheza ulikuwa, Machi 13, 2022 katika Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Coton Sport ya Cameroon dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 na refa huyo alitoa kadi tatu za njano.

Kabla ya happo kwenye mechi ya nyumba iliyozikutanisha Al Ahly ya Misri na El Merrikh ya Sudan, Helder alitoa kadi nne ya njano katika mechi iliyopigwa Machi 5.

SOMA NA HII  'VIBE' LA MASHABIKI YANGA LAWAKUNA MASTAA AFRIKA....TAZAMA WALICHOSEMA...

Rekodi zinaonyesha kadi tatu au nne ni chache kwa mwamuzi huyu kwani, mwaka 2019 alimwaga kadi za njano 14 kwenye michezo miwili ya kimataifa mmoja ulikuwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya ES Tunis ya Tunisia dhidi ya AC Horoya ya Guinea akitoa saba zote sawa na ilivyokuwa kwenye pambano la Kombe la Shirikisho kati ya RSB Berkane dhidi ya Hassania Agadir ambako pia aligawa kadi saba.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alitoa tahadhari kwamba, kwa vile mechi hiyo ndiyo ya kuamua hatma ya Simba, ni lazima mastaa wake kucheza kwa akili na tahadhari kubwa ili kuivusha timu salama.

Mbali na Kanoute na Onyango, wachezaji wengine wa Simba walionyeshwa kadi za njano hadi sasa ni Peter Banda, Erasto Nyoni, Henock Inonga Baka, John Bocco, Bernard Morrison, Pape Ousmane Sakho, Taddeo Lwanga, Meddie Kagere na Aishi Manula.

Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi saba sawa na RS Berkane ya Morocco, wanaoifukuizia Asec Mimosas ya Ivory Coast yenye pointi tisa na US Gendarmarie (USGN) ya Niger ikiwa na pointi tano.