Home Habari za michezo SAIDO ABAKIZA SIKU 40 KUENDELEA KUKIPIGA YANGA…UONGOZI WAMCHUNIA..SENZO AFUNGUKA HAYA…

SAIDO ABAKIZA SIKU 40 KUENDELEA KUKIPIGA YANGA…UONGOZI WAMCHUNIA..SENZO AFUNGUKA HAYA…


Licha ya kuhusika na mabao 11 kati ya 33 yaliyofungwa na Yanga, mshambuliaji Saido Ntibazonkiza anahesabu siku kuondoka katika klabu hiyo inayoongoza Ligi Kuu Bara.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Burundi huenda asimalize msimu huu akiwa Yanga kufuatia mkataba wake kubakisha siku 40 ili kufikia tamati.

Saido alisaini mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika Mei 31, mwaka huu siku chache kabla ya msimu kwisha.

Yanga haijaanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya mchezaji huyo ambaye yupo mguu ndani mguu nje kuendelea na kibarua chake ndani ya klabu hiyo msimu ujao.

“Hakuna mazungumzo yoyote ya Yanga na Saido kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya, hivyo Mei 31 itakuwa ni mwisho wake kuitumikia klabu ya Yanga,” alisema mtu wa karibu na mchezaji huyo.

Saido amekuwa na rekodi nzuri msimu huu baada ya kuhusika katika mabao 11, akifunga sita na kutoa pasi tano za mwisho zilizosababisha mabao.

Katika mechi 11 za Yanga zilizobaki kama atakuwa fiti, basi atahusika katika mechi tano huku akisikilizia mechi ya sita dhidi ya Prisons ambayo haijapangiwa tarehe.

Kama mchezo na Prisons ukipangiwa tarehe, basi mchezaji huyo atahusika katika mechi sita kati ya 11.

Mechi za Yanga zilizobaki ni dhidi ya Simba (Aprili 30), Ruvu Shooting (Mei 4), Namungo (Aprili 23), Mbeya Kwanza (Mei 21) na Dodoma Jiji (Juni 1), Coastal Union (Juni 8), Polisi Tz (Juni 11), Mbeya City (Juni 13), Mtibwa Sugar (Juni 19) na Biashara (Mei 24). Akizungumza hatima ya nyota huyo, kaimu mtendaji mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema anasubiri baraka za benchi la ufundi.

“Sio kwa Saido tu, wachezaji wote watakaoongezewa mikataba watapitishwa na benchi la ufundi,” alisema Senzo akisisitiza kuwa mambo yote ya mikataba yanaendelea ndani kwa ndani na klabu ina utaratibu wa kumalizana na wachezaji au kuiongeza kupitia benchi la ufundi.

“Kwa sasa malengo yetu makubwa kwanza ni kuchukua ubingwa na sio kuota kuzungumzia kuhusu wachezaji.” Wachezaji wengine ambao mikataba yao inamalizika ni Bakari Mwamnyeto, Yassin Mustapha, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Farid Mussa, Kibwana Shomari, Yacouba Sogne na Zawadi Mauya.

SOMA NA HII  WAKATI MAMBO YALIKUWA MAZURI TU...GHAFLA AZAM FC WAMEIFANYIA UKATILI SIMBA KWA BAJANA...