LICHA ya kuanza kuonyesha makali katika mechi mbili zilizopita, nahodha wa Simba, John Bocco ameendelea kuachwa katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inajiandaa na michezo ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zitakazofanyika nchini Ivory Coast.
Stars itaingia kambini Mei 28, mwaka huu kwa ajili ya kuikabili ugenini Niger , hapo Juni 4 na Juni 8, mwaka huu watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuwakaribisha Algeria.
Kikosi kamili cha Taifa Stars kilichoitwa kwa ajili ya mechi hizo mbili ni makipa watatu, Aishi Manula kutoka Simba, Metacha Mnata (Polisi Tanzania) na Abutwalib Mshery wa Yanga huku mabeki ni Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Mzamiru Yassin na Kibu Denis wote kutoka Simba.
Nyota wa Yanga walioitwa Stars ni Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Feisal Salum ‘Feisali Toto’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Farid Mussa.
Wachezaji wengine ni Haji Nonga (Weymouth – Uingereza), Abdallah Kheri (Azam FC), Nickson Kibabage (KMC), Himid Mao (Ghazl El Mahalla ya Misri), Novatus Dismas (Beita Tel Aviv Balyan ya Israel), Aziz Andabwile (Mbeya City), Simon Msuva (huru), Ben Starkie (Spalding, England) Abdul Suleiman (Coastal Union), Reliants Lusajo (Namungo FC), George Mpole (Geita Gold FC) na Ibrahim Koshua (Tusker Kenya).
Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema kutokana na kukosa muda, timu hiyo haitacheza mchezo wa kirafiki kabla ya kuwavaa Niger.
Nsajigwa alisema pia licha ya kukosa timu, wameamua kumuita Msuva kwa sababu wana imani ataisaidia Stars kama alivyofanya katika mechi iliyopita hali ya kuwa hakuna na klabu ya kuitumikia.
“Tumemuita kwa sababu ana mchango mkubwa ndani ya timu yetu ya taifa, pia itamsaidia kuonekana na kupata timu nje ya nchi,” alisema Nsajigwa.
Naye Kocha wa Makipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda alisema wamemuita Mshery kwa ajili ya kumwandaa ingawa anaamini ana uwezo mkubwa wa kucheza endapo atapata nafasi.