Klabu ya Amazulu inayoshiriki Ligi ya Afrika Kusini ‘DStv Premiership’ imekanusha taarifa ya kumtaka aliyekuwa kocha wa Simba, Pablo Franco.
Kupitia mitandao ya kijamii kumekuwa na barua inayosambaa ikiwa na taarifa ya timu hiyo kumtaka kocha huyo ambaye kwa sasa ameachana na Simba kutokana kile kinachodaiwa ni kutofikia malengo ya klabu.
“Kwa wafuasi wetu na nchi kwa ujumla. Tungependa kukuarifu kwamba barua hii na habari inayomhusu kocha wa Uhispania sio ya kweli” ilisema taarifa hiyo kupitia mitandao yao ya kijamii.
Mapema Mei 31 2022 klabu ya Simba ilitangaza kuvunja mkataba na kocha huyo Mhispania aliyejiunga nao November 2021 akitokea Qadsia SC ya Kuwait.
Pablo aliyezaliwa Juni 11, 1980 katika mji wa Madrid, Hispania alianza kucheza soka kabla ya kujitosa kwenye ukocha mnamo mwaka 2009 kama kocha msaidizi kwenye klabu ya Gorcia CF na 2018 akawa kocha msaidizi wa Real Madrid chini ya kocha mkuu Zinedine Zidane ‘Zizzou’.