Kama ratiba itakwenda kama inavyopigwa baada ya Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC, kikosi hicho kitasafiri hadi Boston, Marekani kuweka kambi ya msimu mpya wa michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
Taarifa ziwafikie mashabiki wa Yanga ambao kwa sasa wananenepa kwa furaha kutokana na chama lao kufanya vyema msimu huu, kuwa bilionea na mfadhili wa Yanga, Ghalib Mohamed ‘GSM’ amefurahia mafanikio iliyoyapata na anapiga hesabu kambi ya timu hiyo kwa msimu ujao iwe Boston, Marekani kama chaguo lake la kwanza.
Kambi hiyo itakuwa ni maalumu kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu, ASFC na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo mabosi wanapiga hesabu kufika mbali na walipowahi kufikia watani wao, Simba ambao wamekuwa wakiwatambia kila uchao.
Mbali na chaguo hilo, bilionea huyo pia ana machaguo mengine mawili ikiwamo Uturuki na Afrika, huku Sauzi ikilengwa zaidi.
“Unajua Ghalib (Said) anaipenda sana Yanga na hatua ya kufikia kuwa na nafasi ya kuchukua mataji mawili tena yote yalitokea Simba imemfurahisha zaidi na anataka timu ikaweke kambi huko Boston,” alisema bosi mmoja wa ndani wa Yanga.
“Hiyo ni chaguo la kwanza, tumejaribu kumwambia timu iweke kambi hapahapa Afrika, lakini amekuwa mgumu kukubali na kama sio Marekani basi itakwenda Ulaya mwisho kabisa labda hapahapa Afrika.”
Itakumbukwa msimu uliopita GSM aliipeleka Yanga nchini Morocco katika jiji la kitalii la Marrakech. Hesabu za GSM katika kambi hiyo kwa sasa zinajikita katika ombi la benchi la ufundi ambalo limetaka uhakika wa kupatikana timu nzuri zitakazowapa mazoezi katika mechi za kirafiki kwenye maandalizi hayo.
Benchi la Yanga chini ya kocha Nasreddine Nabi limetaka uhakika huo kutokana na muda mfupi wa kambi.