Unakumbuka lile sekeseke la watumishi hewa lililotokea mwanzoni mwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi chini ya Hayati Rais John Magufuli? Naam! Achana na huko, huku kwenye soka pia kuna watumishi hewa kibao ambao wanavuna mkwanja kwenye timu, lakini kazi yao ni kama haionekani uwanjani.
Tunakuletea baadhi ya majina ya mapro wa kigeni ambao msimu huu wamekuwa kama wafanyakazi hewa ndani ya timu zao kwenye Ligi Kuu Bara.
NURDINI BAROLA (KAGERA SUGAR)
Huyu ni kipa wa Kagera Sugar, raia wa Burkina Faso ambaye msimu huu anaonekana kuwa mfanyakazi hewa licha ya kufanya vizuri misimu mitatu iliyopita akiwa Biashara United pamoja na Namungo.
Barola alitua kwa wakata miwa wa Kagera mwanzoni mwa msimu huu akitokea Namungo alikokuwa amemaliza mkataba aliousaini msimu mmoja nyuma akitokea Biashara United.
Usajili wa Barola kwenda Kagera ulionekana kuwa na tija, lakini mambo yamekwenda ndivyo sivyo kwa kutopata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho na mara nyingi wamekuwa wakidaka kwa kupokezana wazawa Ramadhan Chalamanda na Said Kipao.
YVAN MBALLA (AZAM)
Mwanzoni mwa msimu huu, Azam ikiwa chini ya kocha Mzambia George Lwandamina iliweka kambi Zambia na kurudi na beki Mcameroon Yvan Mballa iliyemsajili kutokea Forest Rangers ya Zambia.
Mballa anayemudu kucheza beki ya kati na pembeni alitua Azam na kuingia kwenye mfumo, lakini hakupata nafasi mara kwa mara ndani ya kikosi cha Lwandamina aliyekuwa akipendelea kuwatumia Lusajo Mwaikenda na Daniel Amoah.
Hata alipoondoka Lwandamina na mikoba yake kuchukuliwa na kocha Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdihimid Moallin mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Mballa kwani hakupata nafasi ya kucheza.
Hadi sasa ligi ikiwa inaelekea ukingoni Mballa ameichezea Azam mechi zisizofika 10 na Aggrey Morris, Abdalla Sebo, Amoah na Lusajo ndio wamekuwa wakipata nafasi ya kuunda ukuta wa matajiri hao wa Chamazi.
ERICK KWIZERA (BIASHARA UNITED)
Baada ya kutemwa na Namungo FC msimu uliopita, Biashara United ilizama mfukoni na kumsajili Mrundi Erick Kwizera kama mchezaji huru. Wakati huo kocha wa Biashara alikuwa Mkenya Patrick Odhiambo, lakini Kwizera anayecheza eneo la kiungo mshambuliaji au winga wa kushoto na kulia alishindwa kufurukuta kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha wanajeshi hao wa mpakani.
Hata alipoondoka Odhiambo na mikoba kupewa Mrundi mwenzake Vivier Bahati mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Kwizera ambaye msimu huu ni kwamba umeisha kwake kwani hata sasa chini ya Khalid Adam hapati nafasi ya kucheza.
CHICO USHINDI (YANGA)
Mwamba huyu alisajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili akitokea nchini DR Congo katika timu ya TP Mazembe.
Wakati Chico anasajiliwa Yanga mashabiki wengi wa timu hiyo walikuwa na matarajio makubwa kwake, lakini hadi sasa mambo yanaenda ndivyo sivyo. Chico ameshindwa kupenya ndani ya kikosi cha kwanza huku majeraha yaliyomuandama yakitajwa kuwa chanzo cha kutofanya vizuri chini ya kocha Mtunisia Nassredine Nabi.
Tangu amejiunga na Yanga, Chico hakuwa na ubora wa kuwashawishi mashabiki wa timu hiyo kumkubali na juzi wakati timu hiyo inatwaa ubingwa mbele ya Coastal Union ndipo alipofunga bao lake la kwanza kwenye ligi katika ushindi wa 3-0.
DEO KANDA (MTIBWA SUGAR)
Mtibwa Sugar katika dirisha dogo la msimu huu ilipotea baada ya kumsajili Mkongomani Deo Kanda kutoka Kitayosce ya Chamnpionship. Wakati Mtibwa inamsajili nyota huyo wa zamani wa TP Mazembe na Simba ilitaka kumtumia ili kumalizia msimu, lakini nyota huyo alikuwa na kesi ya kimkataba na TP Mazembe.
Kesi hiyo iliyokuwa Fifa ilimfanya asicheze mechi yoyote ya mashindano kwa wakata miwa hao hadi pale itakapomalizika na Kanda aliendelea kula maisha Mtibwa. Zikiwa zimebaki mechi nne kumalizika kwa ligi ndipo Fifa imemruhusu kuichezea Mtibwa na alikaa benchi kwa mara ya kwanza kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar ambayo walishinda 3-1.