Kikosi cha klabu ya Yanga kinarejea leo kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa mwisho wa kufungia msimu dhidi ya Mtibwa Sugar mnamo June 29, 2022 katika uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa kumi kamili jioni.
Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Yanga Hassani Bumbuli amesema bado wana kiu ya kusaka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa kimashindano huku kikosi hicho kikitarajiwa kuanza mazoezi rasmi mnamo siku ya Jumanne asubuhi ya June 28,2022.
“Ni mchezo muhimu sana wa kuandika historia,kuna timu ziliweka historia nyuma lakini sisi hatujapoteza katika mashindano yoyote na tunataka kuweka historia ya kumfunga Mtibwa Sugar ili twende tukamalize msimu vizuri Arusha kwenye fainali ya FA”amesema Bumbuli
Mzunguko wa 30 wa ligi kuu Tanzania Bara 2021/22 unatarajiwa kuhitimishwa kwa michezo 8 kuchezwa kwa muda mmoja majira ya saa kumi kamili jioni mnamo June 29,2022 huku klabu ya Mbeya Kwanza kutokea jijini Mbeya ikiwa klabu ya kwanza kushuka daraja kwa msimu huu.
Simba na Azam pekee ndiyo zinarekodi ya kucheza msimu mzima wa mashindano ya Ligi Kuu bila kuruhusu kufungwa hata mechi mmoja, ambapo pia katika misimu hiyo miwili tofauti timu hizo zilitawa ubingwa.