MCHANA wa juzi jiji la Dar es Salaam lilichangamka wakati mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga waliporejea kutoka Mbeya wakiwa na taji lao. Achana na vibe la mashabiki wa klabu hiyo walioipokea timu hiyo iliyokuja pia na Ngao ya Jamii iliyoitwaa Septemba 25 kwa kuinyoa Simba, lakini Yanga ina kila ya sababu ya kujivunia.
Ndio, klabu hiyo yenye umri wa miaka 87 tangu kuasisiwa kwake, juzi ilikabidhiwa taji lake la 28 la ligi na kuifanya iingine kwenye orodha ya klabu namba nne Afrika zenye mataji mengi, nyuma ya Al Ahly ya Misri yenye 42, Esperance ya Tunisia (31) na St George ya Ethiopia yenye mataji 29.
Yanga inakamata nafasi ya nne katika orodha hiyo na timu za Al Hilal ya Sudan na Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyofikisha idadi ya mataji 28 msimu huu kama Yanga.
ILIPOANZIA
Kama hujui ni kwamba Yanga ilizaliwa siku kama ya jana, yaani Jumanne, Februari 11, 1935.
Hata hivyo, historia inaonyesha chimbuko la timu hiyo ilikuwa kati ya mwaka 1926-29 ikiwa na lengo la kisisasa la kuwaunganisha Waafrika katika kudai Uhuru wa Tanganyika.
Inaelezwa kwamba Yanga iliundwa na wananchi wanyonge, wengi wakiwa manamba wa mashambani, wachuuzi na waafrika ambao walikuwa wakitengwa mbele ya watu weupe.
Wanaoifahamu zaidi klabu hii wanasema ilianza kwa jina la Jangwani Boys kisha kuja kuitwa Navigation kabla ya kubadili jina miaka ya 1930 na kujiita Taliana FC.
Hata hivyo mwanzoni mwa 1930, Yanga ilibadilishwa jina na kuwa, New Young na kisha kuasisiwa rasmi mwaka 1935 na miezi michache baadaye timu iligawanyika kwa baadhi ya wachezaji kujiengua na kwenda kuasisi klabu ya Simba iliyozaliwa 1936.
Upo mkanganyiko juu ya tarehe rasmi ya kuasisiwa kwake, baadhi wakisema ni Juni na wengine wakidai ni Februari 11, hata hivyo ni kwamba Yanga ni moja ya klabu kongwe nchini na barani Afrika.
REKODI TAMU
Licha ya kuwa moja ya klabu kongwe nchini, Yanga ambayo ilianza kulitumia jina hilo mwanzoni mwa miaka ya 1970 baada ya agizo la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume aliyezitaka timu zote kuwa na majina ya kiafrika, ina rekodi tamu.
Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na kuandika historia ya kufika robo fainali ikifanya hivyo mara mbili mfululizo, yaani 1969 na 1970.
Kitu cha ajabu ni kwamba Yanga ilifika hatua hiyo na kucheza na Asante Kotoko ya Ghana na moja ya mechi yao iliamuliwa kwa kurushwa kwa sarafu baada ya kushindwa kupata mbabe katika mechi zote mbili za awali.
Achana na rekodi hiyo, Yanga pia ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifanya hivyo mwaka 1998, msimu mmoja tu tangu Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe mfumo wake mwaka 1997.
Pia Yanga inashikilia rekodi ya kuwa klabu pekee mpaka sasa ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa misimu miwili tofauti.
Yanga ilicheza hatua hiyo mwaka 2016 na kurudia tena 2018, ingawa mara zote ilishindwa kuvuka hatua hiyo kwenda robo fainali.
Mbali na rekodi hiyo, Yanga pia ilikuwa klabu ya kwanza Tanzania Bara kucheza robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1995, mwaka mmoja tu baada ya Malindi kufika hatua hiyo 1994.
HATA SIMBA WAMEKAA
Ni kweli Simba ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), wakitwaa taji hilo mara sita, lakini Wekundu hao kwa Yanga wamekaa.
Ndio, licha ya Simba kushikilia rekodi ya kubeba taji hilo mara nyingi, lakini hawajawahi kutwaa nje ya Tanzania, tofauti na Yanga ambao inashikilia rekodi mpaka sasa kwa kufanya hivyo.
Vijana wa Jangwani waliandikia historia kwa kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 1993 nchini Uganda, tena ikienda Kampala kinyonge kulinganisha na watani wao walioenda kwa ndege wakiwa ndio watetezi na kurudi mikono mitupu.
Kama kuna watu waliodhani Yanga ilibahatisha mwaka huo, basi walikosea kwani ilirejea tena rekodi hiyo mwaka 1999 ilipoenda kutwaa ubingwa nchini Uganda kwa mara nyingine.
Rekodi mpaka sasa Yanga imetwaa taji hilo mara tano ikiwa nyuma ya taji moja dhidi ya watani wao, huku Azam FC ikifuatia kwa kulibeba mara mbili, 2015 na 2018.
KATIKA LIGI SASA
Licha ya kubeba mataji matano ya Afrika Mashariki na Kati, lakini Yanga bado ni Baba Lao katika Ligi Kuu ya Bara kwani tangu ilipoasisiwa mwaka 1965 imetwaa ubingwa mara 28.
Wao ndio vinara wakifuatiwa na watani wao waliobeba mara 22 mpaka sasa, lakini pia ndio wababe wa kwanza katika mechi ya watani walipofumua Simba bao 1-0 Juni 7, 1965.
Katika mchezo huo, bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na Mawazo Shomvi kabla ya pambano kuvunjika dakika ya 80 na kugoma kurudiana na watani wao waliokuja kupewa ubingwa mwaka huo wa kwanza kwa kuasisiwa kwa Ligi ya Bara.
Pia kama hujui ni Yanga inayoadhimisha miaka 85 ilikuwa ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani kwa kuifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Juni 1, 1968.
Mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Maulid Dilunga na Saleh Zimbwe waliofunga mawili kila mmoja na Kitwana Manara ‘Popat’.
Hata hivyo, ni Yanga hao hao waliokuja kuandikia historia ya aibu kwa kufumuliwa mabao 6-0 na watani wao Julai 19, 1977 na kwa miaka zaidi ya 40 wanahaha kufuta aibu hiyo bila mafanikio.
Aidha, Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kunyakua ubingwa wa nchi mara tano mfululizo ikifanya hivyo miaka ya 1968-72, japo Simba nayo ilikuja kufanya hivyo baadaye kati ya 1976-80.
Lakini ni Yanga tena waliandika rekodi ambayo mpaka leo haijawahi kufikiwa na timu yoyote katika Ligi Kuu ikiwamo Simba kwa kutwaa mataji mara tatu-tatu mfululizo katika vipindi vitatu.
Ilitwaa mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza mwaka 1991-93 kisha ikarudia tena 1996-98 na 2007-2010, ingawa Simba kwa misimu minne iliyopita ilibeba taji hilo kabla ya kulitema msimu huu, tena kwa aibu kwa kushindwa kukaa kileleni hata mara moja.
ILIFUNIKA KINOMA
Kwa sasa Simba inatambia uwanja wake wa mazoezi uliopo, Bunju, huku Azam wakitangulia mapema kuwa na uwanja wa kisasa, lakini unaambiwa Yanga ndio baba lao toka zamani.
Yanga ndio iliyokuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja wake mwenyewe, walipoujenga Uwanja wa Kaunda, uliokuwa mitaa ya Jangwani na Twiga yalipo makao yao makuu.
Uwanja huo uliifanya Yanga kufunika kwa klabu za Tanzania kwani walikuwa wakitambulisha vikosi vyao kuanzia za watoto, vijana mpaka timu yao kubwa kwenye uwanjani huo.
Pia waliutumia kwa mechi zao mbalimbali za kirafiki kabla ya mafuriko ya mara kwa mara kuwatibulia na kuufanya uwanja huo ufe, japo hivi karibuni walitaka kuufufua upya na kushindikana.
Lakini kama hujui, mbali na uwanja, lakini Yanga pia ndio klabu iliyokuwa na jengo linaloweza kuwahifadhi wachezaji na viongozi wake kwenye makao yao makuu, mbali na kuwa klabu ya kwanza nchini kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wachezaji fedha zao benki.
MAKOMBE KAMA YOTE
Mbali na kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu, Yanga pia inashikilia rekodi kadhaa za kubeba mataji mengine mbalimbali ikiwamo ya michuano ya Ligi Kuu ya Muungano (sasa haipo, iliyoshirikisha timu za Bara na Zanzibar).
Imetwaa michuano ya Kombe la FA mara nne (1975, 1994, 1999 na 2015-16), Kombe la Nyerere, Kombe la Tusker, Kombe la CCM, Kombe la Hedex mbali na kuongoza kwa kubeba Ngao ya Jamii.
NYOTA NJE YA NCHI
Simba kwa sasa inajimwambafai kwa Mbwana Samatta, kucheza Ligi Kuu ya England na kutamba klabu nyingine za Ulaya, huku ikitamba kuwa klabu inayoachia nyota wake wengi kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Hata hivyo, ukweli usiopingika, Yanga ndio klabu ya kwanza kuachia nyota wake kucheza soka nje ya nchi na kutoa mchezaji wa kwanza kucheza soka barani Ulaya.
Kama unabisha, pole yako kwani mwaka 1977 nyota wake, Sunday Manara ‘Computer’, alitimka Uholanzi kupiga soka la kulipwa katika klabu ya Heracles na kumkutanisha na wakali waliotamba enzi hizo duniani kama Ruud Krol, Jaan Rep, Joan Neeskens, Van Hangem na gwiji lao, Johan Cruyff
Mbali na mchezaji huyo, lakini Yanga iliwahi kuwa na Shaaban Nonda ‘Papii’ ambaye amewahi kuwika klabu mbalimbali barani Ulaya, kitu kinachoifanya iwe klabu matata kabisa.