Home Habari za michezo KWA KAULI HII YA AJABU YA MWAKALEBELA KUHUSU CAF…INADHIHIRA MAWAZO NA MITAZAMO...

KWA KAULI HII YA AJABU YA MWAKALEBELA KUHUSU CAF…INADHIHIRA MAWAZO NA MITAZAMO YA YANGA KWA UJUMLA…

 


By MwanaSpoti.

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, mwishoni mwa juma lililopita alitoa kali ya mwaka pale aliposema wataliomba Shirikisho la Soka barani Afrika CAF kuwapangia Yanga kuanzia ugenini kwenye mechi za raundi ya awali ya ligi ya mabingwa Afrika.

Msingi wa kauli hii kwa Mwakalebela ni kwamba Yanga imekuwa waathirika wa ratiba za kuanzia nyumbani, mfano ni mara yao ya mwisho kushiriki, msimu uliopita, ilipokutana na Rivers United ya Nigeria.

Ni ajabu sana kauli kama hii kutoka kwenye mdomo wa mtu wa mpira kama Mwakalebela ambaye CV yake ya kimpira imeshiba kweli kweli.

Kuzaliwa : Machi, 06, 1969

Mahali : Iringa

Elimu : Chuo Kikuu

Uzoefu Kazini

1995 – 2001 : Mshauri wa maswala ya utawala serikali ya Botswana.

2001 – 2006 : Meneja Utawala Mtibwa Sugar kiwanda cha Mtibwa Sugar.

2012-2015 : Mkuu wa Utawala Shirika la Makumbusho ya taifa.

2015 : Mkuu wa Wilaya Wanging’ombe

Uzoefu kwenye Mpira

Katibu wa michezo chuo Kikuu Mzumbe

Mlezi wa Mtibwa Sugar SC

2003-2006 : Mwenyekiti chama cha soka Wilaya ya Mvomero – Morogoro

Mwenyekiti wa Mtibwa United, iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la pili.

Mkurugenzi na Mratibu wa timu ya Mkoa wa Morogoro – Moro Stars kwenye Taifa Cup.

2006 – 2010 : Katibu Mkuu TFF.

2015 : Mratibu wa timu ya Njombe Mji kama kiongozi wa serikali.

2015-2017 : Mjumbe wa kamati ya kuipandisha Lipuli FC.

Kwa CV hii, hawezi kuwa, Mwakalebela hawezi kuwa hajui CAF huwa wanafanyaje kupanga nani aanzie wapi.

Kama mtendaji mkuu wa TFF, tena TFF ya mtu makini kabisa Sir Leodegar Tenga, Mwakalebela hawezi kuwa hajui taratibu za kiutawala hasa ukizingatia yeye mwenyewe pia ni mbobezi katika mambo ya utawala.

Kauli ya Mwakalebela inawakilisha akili, mitazamo na mawazo ya Yanga halisi, achana na Yanga ya Instagram au ya wachambuzi.

Haya ni mawazo halisi ya Yanga Afrika, ambayo inaamini katika ushawishi ili kufikia malengo.

Kama ambavyo Yanga waliweza kuomba mechi yao ya ligi kuu dhidi ya Ndanda, mwaka 2016, ihamishiwe kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam ili wakabidhiwe ubingwa.

Kama ambavyo msemaji wao, Haji Manara alivyomshitaki kwa wamiliki wa EFM Radio, ili mchambuzi Jemedari Said afutwe kazi.

SOMA NA HII  MAYELE AENDELEA ALIPOISHIA ...ATIA KAMBANI GOLI TATU MWENYEWE....AZIZ KI , MAKAMBO WANOGESHA 'SHOW'....

Kama ambavyo walipanga kwenda kwa Mama Samia kumuomba aangalie TFF inavyowaonea.

Kama ambavyo Yusuf Manji kama Mwenyekiti alivyoomba kwa TFF mwaka 2016 Yanga washiriki peke yao mashindano ya Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa sababu walikuwa mabingwa wa ligi kuu na Kombe la Azam Sports.

Mawazo ya Mwakalebela ndiyo yametokea huku. Yeye binafsi Mwakalebela Hana tatizo, ni mtu wa mpira anayejua vizuri taratibu za CAF, lakini taasisi anayoisimamia ina mitazamo yake.

Kwa hiyo tusimhukumu Mwakalebela yeye binafsi, kauli aliyoitoa ni ya taasisi kubwa ya michezo hapa nchini…Yanga Afrika!

Rejea kauli ya Haji Manara mapema mwaka huu aliposema Yanga itanzia raundi ya pili ya hatua ya mtoano kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa sababu wao ni mabingwa wa Tanzania.

Siyo kwamba Haji hajui utaratibu. Haji kabla ya Yanga, alikuwa Simba na miaka yote alikuwa anaona Simba ilikuwa inaanzia wapi.

Msimu wa 2018/19 ilianzia raundi ya awali dhidi ya Mbabe Swallows ya Eswatini, kisha ikakutana na Nkana FC ya Zambia, kisha kufuzu hatua ya makundi…Haji alikuwepo.

Msimu wa 2019/20 ilianzia raundi ya awali na kukutana na ajali ya UD Songo.

Msimu wa 2020/21 ilianzia raundi ya awali na kukutana na Plateau United ya Nigeria kisha kukutana na FC Platinum ya Zimbabwe, kabla ya kufuzu hatua ya makundi…Haji alikuwepo.

Haya yote Haji anayajua alikuwa akiyapigia kampeni kweli kweli kwa kaulimbiu zake za kishujaa kama War In Dar, nk.

Iweje leo ajifanye hajui…siyo yeye, ni taasisi anayoisemea ina mitazamo yake.

Ukiona mambo kama haya yanatoka nje, ujue yamejaa ndani. Yaani maombi kama haya ya Mwakalebela kwa CAF yatakuwa yamefanyika sana hapa nchini katika mazingira ambayo wengi hawayaoni…sasa yanatoka nje hadi CAF.

Ukizoea kula uyoga, ipo siku utakuwa kichuguu…hiki ndicho kinachotokea kwa Yanga.

Yawezekana yale mambo ya kuomba kwa TFF mechi dhidi ya Ndanda ihamishiwe Dar Es Salaam badala ya Mtwara, wanadhani wanaweza kuyapeleka CAF na kuomba mechi yao ya Dar ikaanzie ugenini.

Hiyo ndiyo Yanga Afrika. Daima Mbele!