MWAMUZI Ahmed Arajiga kutokea Manyara ndiye amepewa kuamua mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Yanga na Coastal itakayopigwa kesho Jumamosi kmwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abed jijini Arusha.
Mwamuzi huyo kwa siku za hivi karibuni amekuwa na mwendelezo mzuri katika uamuzi wa mechi na Shirikisho la Soka Tanzania pamoja na Bodi ya Ligi wamekuwa wakimuamini na kumpa mechi kubwa ambazo amekuwa akiziamua kwa kufuata kanuni na sheria.
Miongoni mwa mechi kubwa ambazo Arajiga aliziamua siku za hivi karibuni ni pamja na nusu fainali ya Kombe hili la ASFC iliyoikutanisha Yanga na Simba Mei 28 mwaaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na Yanga kushinda 1-0 na kutinga fainali.
Pia Arajiga anakumbukwa kwa kuchezesha mechi ya fainali ya Kombe hili hili la ASFC mwaka jana baina ya Simba na Yanga iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Taddeo Lwanga.
Hata kabla ya hapo, Arajiga alichezesha mechi ya nusu fainali ya ASFC msimu uliopita kati ya Azam FC na Simba kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea na Simba kushinda 1-0 ikitinga fainali ambapo napo iliichapa Yanga 1-0 na kuwa bingwa kwa msimu uliopita.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Arajiga alipewa beji ya Fifa ya urefa na kumfanya kuwa miongoni mwa waamuzi watatu tu wa kati wa kiume kutoka Tanzania ambao wana beji za kimataifa za urefa wa soka.
Katika mchezo huo, Arajiga atasaidiwa na Mwamuzi msaidizi namba moja Frank Komba wa Dar es Salaam huku namba mbili akiwa Janeth Balama kutoka Iringa. Nassoro Hamduni kutoka Kigoma atakuwa mtathmini waamuzi na Ramadhan Kayoko atakuwa mwamuzi wa akiba.
Katika mchezo huo Yanga inahitaji ushidi ili kupata Kombe la tatu msimu huu baada ya kutwaa Ngao ya Jamii ikiifunga Simba 1-0 mwanzoni kabisa mwa msimu na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku Coastal Union ikitaka Ubingwa huo utakaoifanya kushiriki kuungana na Azam kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.