MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa klabu ya Yanga, Hersi Said amejinadi yeye ni mpambanaji wakati akianza kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Yanga.
Hersi katika uchaguzi wa Yanga katika nafasi ya Urais amesimama kama mgombea pekee.
Mgombea huyo amesema upambanaji huo umetoka kwa wanachama hivyo wampe kura kwa pamoja waitengeneze Yanga.
Hersi akiwa anaomba kura ametaja vipaumbele vyake ikiwemo kuhakikisha inabaki na makombe yake yote matatu na kufanya vizuri kimataifa.
“Nikipata Uraisi nitahakikisha tunakuwa na uwanja wetu pale Kaunda katika makao makuu ya klabu, tuwe na uwanja wa mazoezi Kigamboni,” amesema Hersi na kuongeza;
“Mfumo wa Mabadiliko ambao tayari tulishauanza, kuingiza mapato kupitia wanachama wake lakini vile vile kuhakikisha timu zetu za vijana zote na ya wanawake ziwe imara”.
AJITOFAUTISHA NA GSM
Baada ya kujinadi, Mwenyekiti wa Uchaguzi, Malangwe Mchungahela aliwataka wajumbe kuuliza maswali.
Mmoja wa Wajumbe alimuuliza Hersi kuhusu kujitofautisha nafasi yake ya Urais pamoja na upande wa uwekezaji wa kampuni ya GSM ambayo mgombea huyo ni Mtendaji.
Akijibu swali hilo, Hersi amesema anatambua kama akiwa Rais atakuwa ni msimamizi mkuu wa klabu ya Yanga kwa kupitia mikataba yote hivyo atalazimika kukaa pembeni kwenye mikataba inayohusiana GSM inayohusiana na Yanga.
“Sitokuwa karibu tena na GSM mimi nitakuwa upande wa Yanga kama msimamizi wa klabu, sitohusika na mikataba ya GSM kwa Yanga”. amesema Hersi.