Mabosi wa Simba wanaendelea kusainisha nyota wapya na sasa wamehamishia nguvu zao kwa winga wao wa zamani, Luis Miquissone aliyepo Al Ahly ya Misri.
Simba ilimuuza Luis Al Ahly mwishoni mwa msimu uliopita, lakini hajaonyesha makeke yake kama alivyokuwa Msimbazi na wababe hao wa Afrika inaelezwa wapo mbioni kumtoa kwa mkopo.
Miamba hiyo ya soka inafikiria kumuachia Luis ili wapate nafasi ya kuvuta mchezaji mwingine wa kigeni na Simba baada ya kusikia taarifa hizo, fasta wakatuma maombi kwa Al Ahly kama ikiwezekana wamruhusu aje kukipiga tena Msimbazi.
Simba inamtaka Luis kwa mkopo, lakini ikipanga kumpunguzia mshahara, kitu ambacho kwa sasa kinajadiliwa na miamba hiyo kuona inakuwaje.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa katika ombi lao wamependekeza Luis apunguze mshahara kutoka Dola 50,000 (zaidi ya Sh 100 milioni) kwa mwezi na kuwa isiyozidi dola 15,000 (zaidi ya Sh 30 milioni).
Mmoja wa mabosi Simba alisema mkataba wa Luis na Al Ahly una kipengele kinachoeleza kama atauzwa au kutolewa kwa mkopo hapa Tanzania, Simba ndio inapewa nafasi ya kwanza labda ikatae wenyewe na hilo linafanana na suala kama lile la Clatous Chama.
“Tumewapa maombi yetu tunamtaka Luis kwa mkopo kwani si rahisi kumnunua gharama yake ni kubwa ila kwenye mkopo huo tumewaomba uongozi na mchezaji tutakuwa na uwezo wa kulipa mshahara wa Sh30 milioni kwa mwezi na si kama ule anayopata wakati huu,” alisema bosi huyo na kuongeza;
“Kama Luis na uongozi wake watakubaliana kupunguza huo mshahara tupo tayari kumrudisha kikosi ila kama ikishindikana kutokana na hayo maslahi ni wazi atakwenda nchi nyingine na si Tanzania tena.
“Kuna timu kutoka nchi mbalimbali kama Sudan, Afrika Kusini na nyingine zenye asili ya Kiarabu zimeonyesha nia ya kumtaka Miquissone na wameweka pesa nyingi zaidi yetu kwahiyo lolote linaweza kutokea mbali ya kuwapatia maombi hayo.
Kigogo huyo alisema kwa sasa ni ngumu kwao kuzungumza na Luis kwa vile bado yupo kwenye mkataba mrefu na Al Ahly, ila kwa vile walivyoishi naye anatambua thamani ya klabu hiyo ya Msimbazi na huenda akarudi kucheza.
Kama Simba imepanga kama itampata Luis basi itamtafutia mahali pa kwenda na mkopo kwa Peter Banda na kama itashindikana basi Banda atasalia kwa msimu ujao.
Wakati hilo likiendelea Simba itakamilisha usajili wake wa msimu huu kwa kumnasa nyota wa nane beki wa kati aliyewahi kufundishwa na kocha mpya, Zoran Maki katika kikosi cha Wydad Casablanca ya Morocco.
Simba hadi sasa imekamilisha usajili nyota saba, Nassoro Kapama, , Vicent Akpan, Moses Phiri aliyetambulishwa tayari, Augustine Okrah, Nelson Okwa na Cesar Lobi Manzoki, Habibu Kyombo.
Meneja habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kweli timu yake imeonyesha nia ya kumrudisha Miquissone na kufuata njia sahihi za usajili ikiwemo mawasiliano na uongozi wa Al Ahly ili kumpata hata kwa mkopo.