Home Habari za michezo ISHU YA MKATABA WA MANULA NA SIMBA …USIRI MKUBWA WATAWALA…MABOSI MSIMBAZI WAPANGA...

ISHU YA MKATABA WA MANULA NA SIMBA …USIRI MKUBWA WATAWALA…MABOSI MSIMBAZI WAPANGA KUSHTUA MIOYO YA WATU…


KUKIWA na usiri mkubwa ndani Bodi ya Wakurugezi ya Simba, chini ya Mwenyekiti wake, Salim Abdallah ‘Try Again’, imemwongeza mkataba mpya wa miaka miwili kipa chaguo la kwanza wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Aishi Manula.

Lakini pia klabu hiyo imewataka mashabiki wake kutulia kwa sababu imewaandalia mambo mazuri na makubwa katika msimu mpya.

Manula alikuwa amemaliza mkataba na klabu hiyo na tayari sintofahamu ya hatima yake ilianza kuzua taharuki na sasa mabosi wa Simba wamemalizana na mlinda mlango huyo wa zamani wa Azam FC.

Taarifa za uhakika zinasema Simba imemalizana na Manula na sasa ataendelea kuwa sehemu ya nyota wanaoitumikia klabu hiyo.

Chanzo hicho kilisema uongozi umejipanga kumpa heshima Manula kwa kuandaa utambulisho unaofanana na thamani yake katika muda muafaka ambao utapangwa.

“Ni kweli Aishi hayuko katika kikosi cha Simba huku Misri, lakini sio kwamba hayuko ndani ya timu hiyo bali yuko katika majukumu ya Stars, akimaliza ataungana na Simba kwa sababu ameshaongeza mkataba wa miaka miwili,” kilisema chanzo chetu.

Taarifa zaidi zilisema Manula alitamani kupata timu nje ya Tanzania, lakini tatizo linalokwamisha kuondoka ni ofa ndogo ambazo zinakuja lakini pia hahitaji kwenda kukaa benchi huko atakapotua.

Manula alisema ni kweli mkataba wake na Simba umemalizika na sasa ameweka mbele nguvu na akili kuitumikia Stars.

“Mkataba na Simba umemalizika na bado sijasaini mkataba timu yeyote, ila kama nitaongeza au kusaini sehemu yoyote litawekwa wazi,” alisema Manula.

Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliwataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu na hivi karibuni wataweka wazi majina ya  wachezaji ambao wamewaongezea mikataba na walioachana nao.

Aliongeza zoezi la kutikisa nchi litaendelea kwa kutambulisha wachezaji wao wapya waliowasajili wakiwa kambini Misri.

“Wanasimba wasiwe na presha juu ya usajili, uongozi uko makini kwa wachezaji ambao wanaendelea kubaki katika timu lakini pia kuhakikisha lile zoezi letu la usajili linaendelea kutambulisha mchana kweupe.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA TABIA ZAKE KUWA SIO...MORRISON APEWA MASHARTI MAPYA YANGA...NABI AKOMAA NAYE...

“Kuhusu Mhilu (Yusuph), bado anaendelea na mazungumzo na uongozi, na wakifanikisha au kuelewana, basi mustakabali wake ndani ya Simba utawekwa hadharani,” Ahmed alisema.

Kiongozi huyo aliongeza hali ya wachezaji wa Simba walioweka kambi Misri iko vizuri na jana jioni walitarajiwa kuanza mazoezi ya kujiwinda na msimu mpya utakaoanza Agosti 17, mwaka huu.

“Timu kubwa kwenye mazingira bora ya kujiandaa kufanya makubwa katika msimu mpya,” alisema Ahmed.