Mshambuliaji kiongozi wa klabu ya Yanga, Fiston Kajala Mayele ‘Mzee wa Kutetema’ amesema amerejea tena katika kambi ya timu yake ili kujiunga na wachezaji wenzake katika maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2022/23.
Mayele ambaye ni mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita na mfungaji wa pili wa Ligi Kuu ya NBC akiwa na mabao 16 amekiri kupokea ofa ya timu kubwa barani Afrika ambazo zilikuwa zikitaka huduma yake huku akiitaja Kaizer Chiefs kuwa ndio timu iliyofikia hatua nzuri za kutaka kumsajili.
Kuhusu kurejea Kambini
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kurejea kwa mara ya pili tena. Tunaanza preseason, najua ni wakati mgumu lakini ukifanya preseason nzuri na msimu wako utakuwa mzuri pia. Mimi ni siku ya kwanza leo kuwa na timu lakini nilikuwa nafanya mazoezi kwetu Lubumbashi,” amesema Mayele.
Kuhusu kuondoka Yanga
“Ni kweli timu zilikuwa nyingi zilizotaka kunisajili, lakini timu iliyokuwa imekaribia kunisajili ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Al Hilal ya Sudan na Raja Casablanca ya Morocco.
“Mimi bado ni mchezaji wa Yanga, nilisaini mkataba wa miaka miwili, nimemaliza mwaka mmoja hivyo bado mwaka mwingine mmoja. Na hili nataka niliweke sawa, kwa sababu nasiki wanasema niko Yanga kwa mkopo, hapana, mimi nilisajiliwa Yanga kwa miaka miwili, kwa sasa bado mwaka mmoja,” amesema Mayele.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania viliripoti kuwa Mayele amekamilisha mazunguzo na Kaizer na wakati wowote angejiunga na timu hiyo na ndio maana hakuwa kambini huku wengine wakienda mbali zaidi na kudai kuwa Mayele yupo nchini Afrika Kusini kumalizana na Kaizer.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga umeshatoa kauli mara kadhaa kuwa wachezaji wake akiwemo Mayele na Feisal Salum ‘Fei Toto’ hawauzwi kwa sasa kwani wapo kwenye mipango ya mwalimu msimu ujao.
Aidha, kuhusu nini Wanayanga wakitegemee kutoka kwa Mayele msimu huu amesema; “Naweza kuwaambia kwamba msimu uliyopita umepita, hivyo kwa sasa kama timu tunafanya maandalizi ya msimu mpya na ndio maana nimerejea kambini kujiunga na wenzangu, nikifanya mazoezi vizuri na msimu wangu utakuwa mzuri, tunaamini kwa maandalizi mazuri ya preseason tutakuwa na msimu mzuri kwa uwezo wa Mungu,” amesrma Mayele.