Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZA KAZI YAKE KWA YANGA MSIMU HUU…NABI AIBUKA NA KUVUNJA...

BAADA YA KUMALIZA KAZI YAKE KWA YANGA MSIMU HUU…NABI AIBUKA NA KUVUNJA UKIMYA KUHUSU YA MSIMU UJAO…


WAKATI kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Yanga kikiwa katika mapumziko, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nesredine Nabi amesema wanatakiwa kujipanga zaidi kwa sababu msimu ujao utakuwa mgumu kuliko ilivyokuwa katika msimu uliomalizika.

Nabi alisema amewapa wachezaji wake mapumziko ya wiki mbili na wakirejea wataanza upya kujiwinda na msimu mpya ambao pia malengo yao ni kuona wanatetea mataji yote matatu waliyoshinda.

Nabi alisema anaamini msimu ujao ambao utaanza na mchezo wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hautakuwa mwepesi.

Kocha huyo alisema wamejipanga kuongeza umakini na kuwaandaa wachezaji wajitume kwa sababu hakutakuwa na muda wa kujiuliza walipokosea.

“Wachezaji wamefanya kazi kubwa na nzuri msimu huu kuchukua mataji yote matatu si kazi ndogo, wanahitaji kupumzika pamoja na familia zao ikiwamo kupongezana, ila haitakuwa zaidi ya wiki mbili,” alisema Nabi.

Aliongeza wachezaji wanastahili kupata muda wa kutosha zaidi, lakini muda wa likizo umekuwa mfupi kwa sababu wao pia wanashiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yapo karibu na hawahitaji kutolewa mapema.

“Wachezaji wanatakiwa kutumia vizuri huu muda wa mapumziko, nataka wakirejea kila mmoja awe makini na kufanya mazoezi, kwa sababu tutakuwa na mazoezi magumu katika siku za mwanzo za maandalizi ya msimu mpya,” alisema Nabi.

Alieleza wanatarajia ‘pre season’ yao itaanza kwa nguvu na wachezaji watafanya mazoezi yenye kasi kubwa ili kuendelea kupata matokeo mazuri katika mashindano yote watakayoshiriki.

“Tunataka kuendelea pale tulipoishia msimu huu ambapo malengo yetu yalikuwa ni kuwapa raha mashabiki waliokuwa pamoja na timu kwa kipindi chote hadi tuliposhinda mataji matatu,” Nabi alisema.

Alieleza anahitaji kuona kila mchezaji anaongeza umakini na yeye atakuwa mkali kwa nyota wake wote ili kufanikisha mipango mipya aliyoiandaa kuelekea msimu ujao unaotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 17, mwaka huu.

Alisema amejiandaa na anafahamu mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 13, mwaka huu dhidi ya watani zao Simba ambayo ni ‘Derby’ ya Tanzania utakuwa mgumu, hivyo anatakiwa kuandaa taswira tofauti na iliyozoeleka.

SOMA NA HII  ZIGO LA MASKANI POA LIMERUDI TENA NDANI YA DStv...SAFARI HII MAINJINIA NI WAPYA...MSELELEKO NI ULE ULE TU KITONGA...

“Kuhusu usajili sina mashaka kabisa na viongozi, matarajio makubwa ya kufanya kile nilichowaambia katika taarifa ya usajili yatatimia kwa ajili ya kuimarisha timu yetu iweze kupambana kwenye ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa,” alisema kocha huyo.

Yanga imeweka rekodi ya kumaliza msimu wa 2021/2022 bila kufungwa mechi hata moja, hivyo inataka kuona inaendeleza ubabe huo katika msimu mpya.

Ili kufikia malengo hayo, inaendelea kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji nyota na tayari imeshamtangaza kumrejesha klabuni kwake winga wa kimataifa kutoka Ghana, Bernard Morrison aliyekuwa akiichezea Simba.