Home Habari za michezo KUHUSU ISHU YA MAYELE KUTAKIWA KAIZER CHIEF….NABI AFUNGUKA A-Z DILI ILIVYO NA...

KUHUSU ISHU YA MAYELE KUTAKIWA KAIZER CHIEF….NABI AFUNGUKA A-Z DILI ILIVYO NA UKWELI WA MAMBO…


Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi tayari ameshatua nchini juzi tayari kuanza maandalizi ya msimu mpya, huku akiwashusha presha mashabiki wa timu hiyo kuhusiana na tetesi za kuondoka kwa mshambuliaji wao tegemezi, Fiston Mayele.

Tangu kumalizika kwa ligi kumekuwa na tetesi kwamba nyota huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC anatakiwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini jambo ambalo limewapa hofu mashabiki wa timu hiyo kutokana na mafanikio aliyowapa mshambuliaji huyo aliyemaliza nafasi ya pili akifunga mabao 16 kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Nabi alisema kuwa mipango yao ni kufanya vizuri na kufika mbali kwenye michuano yote watakayoshiriki hivyo hawana mpango wa kumwachia mshambuliaji huyo sababu yupo kwenye mipango yao.

“Niwatoe hofu mashabiki wa Yanga kwamba Mayele bado ni mchezaji wetu na atakuwa nasi mpaka mwisho wa msimu mkataba wake utakapomalizika, binafsi nimeongea naye na kesho atakuwa mazoezini na wenzake kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao,” alisema Nabi.

Kocha huyo ameeleza kuwa yeye kama kocha mwenye kuhitaji mafanikio ni vigumu kuruhusu mchezaji huyo kuondoka kutokana na mchango wake ndani ya timu, imani yake nikwamba alichokifanya msimu uliopita msimu ujao utakuwa mara mbili yake kutokana na kikosi chao kuimarika zaidi kutokana na usajili walioufanya.

Aidha, kocha huyo raia wa Tunisia ameeleza kuwa maandalizi yao amepanga kufanyika kwa usiri mkubwa sababu anataka kutumia vyema muda uliopo kwa ajili ya kujenga timu itakayocheza soka lenye mvuto na kumtaabisha mpinzani.

Alisema msimu uliopita timu yake pamoja na kutwaa mataji yote bila kupoteza mchezo lakini haikufikia kwenye kiwango alichokihitaji hivyo msimu huu amepanga kutimiza ahadi hiyo ili kuthibitisha ubora wa kikosi walichonacho hivi sasa.

Yanga imeamua kubaki Avic Town Kigamboni kwa ajili ya kambi hiyo ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, kazi kubwa kwa Nabi ni kuhakikisha timu hiyo inatetea mataji yote ya ndani na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SOMA NA HII  BARBARA AVUNJA UKIMYA ISHU YA USAJILI WA KINA SHIBOUB...ATAJA SAPRAIZI....