Aliyekuwa Kocha Mkuu wa miamba ya Soka Barani Afrika, Al Ahly ya Misri, Pitso Mosimane raia wa Afrika Kusini amesema tukio la parade ya Yanga kusherehekea Ubingwa wa NBC limetoa funzo kwa vilabu vingi vya bara la Afrika kuwa inawezekana kufanya vile sio mpaka Ulaya pekee.
Pitso amesema hayo jana Ijumaa, Agosti 5, 2022 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam baada ya kukaribishwa na Klabu ya Yanga katika tamasha la Kilele cha Wiki ya Wananchi litakalofanyika kesho katika Dimba la Mkapa.
“Nimekuwa na shauku ya kushiriki Wiki ya Wananchi na napenda kuwapongeza Young Africans Sc na Rais Hersi Said kwa kushiriki matukio ya kijamii na kuinua soka la vijana na pia nipende pia kumpongeza Kocha na Benchi lake la ufundi kwa kushinda Makombe Matatu.
“Niliona hamasa kubwa ya mpira kwenye Sherehe za Ubingwa (parade) kwa Mashabiki wa Klabu hii pendwa na hamasa hii ilipelekea Dunia nzima kuangalia kile walichofanya Yanga kwenye mapokezi ya Ubingwa na ilinivutia kupita kiasi,” amesema Pitso.