Mabadiliko iliyoyafanya Yanga katika mchezo dhidi ya Coastal Union katika moja ya mechi za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, yametajwa kuvunja kanuni, huku mwamuzi wa mechi hiyo, Raphael Ikambi akisubiri hatma yake kwenye kamati.
Bodi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (IFAB) inayoongozwa na rais wa FIFA, Gianni Infantino katika mkutano wake mkuu wa 136, Doha, Qatar iliridhia mabadiliko na ufafanuzi wa sheria kwa msimu wa 2022/23, ambayo yalianza kutumika Julai Mosi, ikiwa ni pamoja na idadi ya wachezaji ambao wanatakiwa kufanyiwa mabadiliko (sub).
Ilipitishwa kutoka wachezaji watatu hadi watano, huku katika kufanya sub na kutakiwa kuingia kwa awamu isiyozidi tatu na kukiwa na kipengele kuwa inaweza kuongezeka kama itatokea mchezaji atakumbana na kadhia ya kuumia vibaya hasa kichwani kiasi cha kuhatarisha uhai wake.
Kwenye mechi dhidi ya Coastal, licha ya kutokuwepo kwa tukio lolote la ajali ambalo lilihatarisha uhai wa mchezaji, kocha Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko kwa awamu nne dakika ya 25, 55, 71 na 83, wakitoka Jesus Moloko aliyeshindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia mguu, Heritier Makambo, Bernard Morrison na Aziz Ki na kuingia Dickson Ambundo, Fiston Mayele, Farid Mussa na Gael Bigirimana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni alisema tukio hilo amelisikia na kama kweli limetokea basi kanuni zimevunjwa.
“Sijaliona tukio hilo, ingawa nimelisikia, kama ni kweli ndicho kimetokea basi kanuni zimevunjwa na kamati husika italichukulia hatua kwa mwamuzi, lakini tu ikibainika kuwa ni kosa, ingawa katika matokeo ya mechi haitaathiri chochote,” alisema Hamduni.
Mwamuzi, Israel Nkongo alisema kama Yanga ilifanya mabadiliko kwa awamu nne katika mchezo huo, basi mwamuzi wa mechi hakuwa makini katika kusimamia kanuni.
“Inaweza kufanyika mara nne, lakini itategemea kama mchezaji atakumbana na kadhia ya kuumia vibaya hasa kichwani kiasi cha kuhatarisha uhai wake, kinyume na hapo ni kosa,” alisema Nkongo.
Tukio kama hilo limewahi kutokea wakati wa kuwaniwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, hatua ya mtoano, kati ya DR Congo dhidi ya Benin, suala lililoamuliwa na FIFA, na hakuwa na hatua zozote zilizochukuliwa kwa timu, zaidi ya mwamuzi kuingia matatani.
Rufaa hiyo ya Benin ilikuwa juu ya DR Congo, ambayo ilishinda kwa mabao 2-0, kufanya mabadiliko kwa awamu nne kinyume cha kanuni hiyo.
Kulingana na ripoti ya mechi, DR Congo ilifanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 63, ilipokuwa mbele kwa bao 1-0. Mabadiliko mengine mawili ilifanywa baada ya bao la pili dakika ya 77 na kisha dakika ya 84, kabla ya mchezaji wa mwisho kuingia dakika za majeruhi mwishoni mwa mechi.Yanga hadi sasa imecheza 37 bila ya kipigo tangu ilipochapwa na Azam FC 1-0, kwa bao la shuti la mbali la Prince Dube kwenye Uwanja wa Mkapa Aprili 25, 2021.
Mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72, Steven Mguto alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu tukio hilo hadi pale watakapoitisha kikao cha kamati.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote hadi pale tutakapoitisha kikao cha kamati, angalia kwanza kanuni zinasemaje kuhusu hilo,” alisema Mguto.