Kocha wa makipa wa Yanga, Mbrazili, Milton Nienov, ameweka wazi kuwa, ndoto yake ni kuona anafikia rekodi aliyoiweka akiwa na Simba ya kufika angalau robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Mbrazili huyo ameweka wazi kuwa, wana nafasi kubwa ya kufikia mafanikio hayo kutokana na ubora wa kikosi walichonacho msimu huu.
Katika michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga wamepangwa kuanzia hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini.
Nienov msimu wa 2020/21 alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichotolewa na Kaizer Chiefs hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kupigwa chini Oktoba mwaka jana na kuibukia Yanga.
Nienov alisema: “Nikiwa na Simba katika mashindano haya nilifanikiwa kufika robo fainali tena kwa mafanikio makubwa ya kuongoza hatua ya makundi dhidi ya bingwa mtetezi Al Ahly.
“Kama mtu ambaye naamini sana katika kufanikiwa naweza kusema ni ndoto yangu kuona naipigania Yanga kufikia mafanikio kama hayo, naamini kwa ubora wa kikosi ambacho tunacho tuna nafasi kubwa ya kufanya hivyo japo hatuna presha kubwa sana juu ya hilo kwani lengo mama ni kufika angalau hatua ya makundi.”