Yanga imecheza mchezo wa kwanza wa kirafiki wa kujipima nguvu tangu kusimama kwa Ligi Kuu Bara na kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya KMC.
Katika mchezo huo ambao umechezwa katika Uwanja wa Avic Town ambao Yanga wanautumia kwenye mazoezi yao mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna aliyefanikiwa kupata bao.
Kipindi cha pili Yanga walirejea na nguvu kubwa na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka akitangulia winga Bernard Morrison kupachika bao la kwanza akipokea pasi ya beki wao wa kulia Djuma Shaban.
Yanga wakaongeza bao la pili kupitia kiungo mkabaji Gael Bigirimana akitumia pasi ya Morrison.
KMC wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia Sadala Lipangile akitumia makosa ya mabeki wa Yanga.
Yanga imekuwa katika mazoezi makali kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC utakaopigwa Septemba 6 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.