KOCHA wa Simba, Zoran Maki ameanza kuwaelewa mastaa wake wawili, Victor Akpan na Nassoro Kapama.
Kwa mara ya kwanza waliitumikia timu hiyo juzi Jumapili usiku kwenye mchezo wa kimataifa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana nchini Sudan.
Zoran alisema anahitaji kuwapa mechi nyingi Akpan na Kapama kutokana na viwango vyao walivyoonyesha katika mechi hiyo kuna maeneo mengi wamemshawishi na kuendelea kuwaamini.
Zoran alisema Akpan alikuwa imara katika eneo la kiungo alifanya kazi nzuri ya kukaba na kuzuia mashambulizi pamoja na viungo wa timu pinzani na muda mwingine alikuwa akianzisha mashambulizi.
Alisema kuna wakati alichukua mipira chini na kuanzisha mashambulizi kutokana na pasi zake za kwenda mbele na muda mwingine alisogea hadi nusu ya wapinzani kulingana na shambulizi lilivyo.
“Kuhusu Kapama amecheza vizuri katika eneo la beki wa kati pamoja na Henock Inonga kana kwambwa walishawahi kucheza pamoja huko nyuma ingawa kuna makosa ya kiulinzi aliyafanya ikiwemo ile penalti lakini mengi yanarekebishika tena kwa haraka,” alisema Zoran.
Katika hatua nyingine Zoran alisema kuna makosa yalifanyika kama timu lakini Akpan na Kapama akiwapa mechi zaidi anaamini watakuwa katika viwango bora zaidi ya walichoonyesha katika mchezo huo.
“Niliamua kutumia mfumo wa 3-5-2 kwani kuna baadhi ya mechi hasa za kimataifa tutahitaji kucheza kwa nidhamu kubwa ya ulinzi kutokana na wapinzani walivyo hasa tukiwa ugenini,” alisema Zoran na kuongeza;
“Nimeutumia mfumo huu kwa mara ya kwanza tangu nifike Simba ila wachezaji wote wameweza kuelewa na kuufanyia kazi kama vile ambavyo nilikuwa nahitaji hadi nikapata ushindi,” alisema Zoran