Uongozi wa Simba jana mchana ulitangaza kuvunja mkataba na kocha wake Mserbia Zoran Manoljović (60) baada ya kudumu kwa miezi miwili huku sababu tatu zikitajwa kumuondoa.
Huyo ni kocha wa pili wa kigeni kutimuliwa tangu kuanza kwa msimu huu, mwingine ni kaimu Kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin raia wa Somalia na Marekani.
Simba ilimuajiri na kumtangaza kwa mbwembwe Zoran Juni 28, mwaka huu akichukua nafasi ya Mfaransa, Franco Pablo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa mabosi wa timu hiyo, sababu tatu za msingi ambazo zimemuondoa kocha huyo kuendelea kukinoa kikosi hicho huku mshambuliaji wa timu hiyo, Mserbia Dejan Geogjivic akipewa muda wa kuangaliwa.
Bosi huyo alizitaja sababu hizo ya kwanza ni “Kuishiwa mbinu, kocha kwa siku zote alizokaa na timu hiyo akiifundisha ameonekana kuishiwa mbinu za kuipa matokeo mazuri ya ushindi katika michezo waliyoicheza.
“Timu imeonekana kucheza soka la kawaida ambalo haliendani na hadhi yetu, Simba sio timu ya kucheza soka la kujilinda muda wote, tulishazoea tukicheza soka la pasi na kushambulia.
“Pili, wachezaji kukosa furaha wakiwa kambini, mazoezini na katika michezo miwili ya ligi ambayo tumeicheza, licha ya kupata ushindi katika michezo hiyo.
“Hili la wachezaji kukosa furaha tumeona lingetuathiri katika ligi, kwani wachezaji ndio wanaopambana katika timu, hivyo tungeendelea kubaki naye basi angetuvurugia mipango yetu ya ubingwa.
“Tatu, Timu kukosa utulivu inapokuwepo uwanjani ikicheza, hivyo hilo tumeliona tangu tukiwa katika pre season na kuamua kuchukua maamuzi magumu ya kuachana naye,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo Mtendaji wa timu hiyo, Barbara Gonzalez alithibitisha kuvunja mkataba wa miaka miwili wa kocha huyo mara baada ya kutoa taarifa ya klabu.
“Ni kweli tumeachana na Zoran, na mipango yetu kuwa na kocha wa mipango ya muda mrefu katika projekti yetu na sio kuwa na kocha mtalii.
“Na ninaamini mara baada ya taarifa hii, nitapokea maombi mengi ya makocha kutoka Ulaya kwa kutumia CV zao na sio Afrika. Katika ukanda huu Afrika wapo makocha wengi wa Afrika waliofanya vizuri na kufanya makubwa katika Kombe la Dunia.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika, wapo makocha watano Ukanda wa Afrika waliowezesha nchi mbalimbali kufuzu Kombe la Dunia ambao wanastahili kuja kuifundisha Simba na baadhi yao ni Jalel Kadri (Tunisia), Otto Addo (Mghana), Walid Regragui (Morocco), Aliou Cisse (Senegal) na Rigobert Song (Cameroon),” alisema Barbara.
Naye Meneja wa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa Haraka wameanza mchakato wa kumpata kocha mpya atakayekuja kuanza kazi kabla ya kuanza kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Jumapili hii.
Katika hatua nyingine, Zoran juzi alitambulishwa kama Kocha Mkuu wa Klabu ya Ittihad ya nchini Misri.