Kueleka mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini utakaopigwa keshokutwa Jumamosi, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amepiga mkwara mzito akisema kikosi chao kitatoboa na hakuna wa kuwazuia.
Septemba 10, mwaka huu, Zalan watakuwa wenyeji, mechi ikitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, kisha Septemba 17, Yanga watakuwa wenyeji kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Juzi Jumanne, Yanga ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Injinia Hersi amesema mechi hiyo imewapa mazoezi tosha.
Hersi alisema: “Binafsi nadhani lilikuwa jambo la muhimu kupata mchezo dhidi ya Azam kabla ya kucheza na Zalan, hii ni kutokana na ubora na maswali magumu ambayo Azam walituuliza, lakini sasa tumefunga mjadala wa Azam na tunajipanga na mchezo dhidi ya Zalan.
“Malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunashinda mchezo huu na kufuzu hatua inayofuata, tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi lakini niseme tumekamilisha maandalizi yote na tuna imani kubwa ya kufuzu hatua inayofuata.”