Watanzania wanaoishi nchini Malawi wameonesha matumaini kwa Simba kushinda mchezo wao wa mkondo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Nyassa Big Bullet, huku wakitoa angalizo kwa mastaa wa Wekundu hao.
Pia wamewataja baadhi ya wachezaji wanaoweza kuamua mechi na kuipa ushindi Simba ikiwa ni Clatous Chama, Augustine Okrah na Dejan Georgjevic.
Wakizungumza wakati wa mazoezi ya Simba kwenye uwanja wa Bingu jijini hapa, watanzania hao wakiwamo mashabiki wa Yanga wamesema Simba inaweza kushinda lakini kazi si ndogo kutokana na mwenendo wa wapinzani wao katika mechi zao za Ligi Kuu nchini Malawi.
Miraji Mshama shabiki wa Simba ambaye anaishi nchini hapa amesema Simba ina wachezaji wenye ubora lakini Nyasa Big Bullet wanawategemea sana vijana chipukizi.
“Kwenye mechi yao mojawapo katika Ligi Kuu wameshinda 8-0 hivyo Simba wasidharau kuna upinzani mkali ukizingatia wapo ugenini” amesema Mshamu.
Naye Modrick Hamis ambaye ni shabiki wa Yanga, amesema kwa sasa anaisapoti Simba kwani ndio wanaiwakilisha nchi na kwamba Wekundu hao wanapaswa kuwa makini kutafuta mabao ya mapema huku akibainisha kuwa iwapo Dejan ataanza katika mechi hiyo anaweza kufanya vizuri kwani hali ya hewa inaruhusu.
“Kwa sasa nauweka Uyanga mfukoni kuisapoti Simba, niwashauri kuwa makini kipindi cha kwanza wapate mabao ya haraka lakini pia wakimuanzisha Dejan anaweza kufanya vizuri, nimemfuatilia vyema” amesema Hamis.
Naye Ally Hassan amesema wana matumaini makubwa na timu yao na kwamba wachezaji Okrah na Chama wanaweza kuwapa raha mashabiki wa Simba.
“Mbio za Okrah na uwezo alionao Chama katika kuchezesha timu inaenda kutupa ushindi Simba, tunaamini kesho tutapata furaha” amesema Hassan.