Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU…HIVI NDIVYO PESA ZA GSM ZINAVYOISINZISHA SIMBA KILA WAKIKUTANA NA YANGA…

UKWELI MCHUNGU…HIVI NDIVYO PESA ZA GSM ZINAVYOISINZISHA SIMBA KILA WAKIKUTANA NA YANGA…

Habari za Simba leo

Nyakati zimekwenda wapi? Ni swali gumu mno kuweza kulijibu kwa sasa. Nyakati zimekwenda kasi sana na Simba sasa amekuwa mteja wa Yanga tena. Inashangaza sana.

Tangu kutimia kwa karne ya 21 Simba amekuwa mbabe wa Yanga katika kila eneo. Simba iwe mbovu ama nzuri haikuwahi kusumbuliwa na Yanga katika karne hii ya 21. Kwa nini? Twende taratibu nitakueleza.

Simba iliweza kuikamata Yanga katika kila idara. Yanga ilipambana usiku na mchana lakini haikuweza kutawala Dabi ya Kariakoo hata siku moja.

Kuna baadhi ya watu walidhani pengine ni umasikini ulisababisha wao kufungwa na Simba kila mara, lakini hapana. Hata wakati wa Yusuf Manji, bado Simba isiyokuwa na fedha iliisumbua Yanga.

Katika miaka yote 11 ambayo Manji alikuwa mfadhili na kisha Mwenyekiti wa Yanga, bado Simba ilitawala hizi mechi za Dabi ikiwa haina tajiri wa kueleweka. Unajua kwa nini?

Ni hawa watu walioitwa Friends of Simba. Ni kundi la watu wenye mapenzi ya dhati na Simba ambao wana uwezo kiasi na nguvu serikalini. Hawa waliifahamu vizuri Dabi ya Kariakoo na kujua namna ya kuicheza.

Hili ni kundi lililokuwa likiongozwa na Evans Aveva, Dioniz Malinzi, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na marehemu Zakaria Hans Poppe. Ni kundi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye soka la Tanzania. Sehemu kubwa ya kundi hili ndilo linaloongoza Simba kwa sasa.

Hawa kina Mulamu Nghambi, Salim Abdallah ‘Tryagain’, Mohammed Nassoro ‘Mkigoma’, Musley Ruweiy, Kassim Dewji na wengineo ni Friends of Simba.

Ni Hans Poppe pekee ametangulia mbele za haki, lakini wengi wapo. Sasa nini kimebadilika? Kwa nini Friends of Simba waliweza wakiwa na Simba dhaifu, lakini sasa imekuwa ngumu kushinda wakiwa na timu imara?

Simba imeshinda Dabi moja tu kati ya nane za mwisho. Mara ya mwisho kwenye ligi kupata ushindi mbele ya Yanga ilikuwa mwaka 2019. Ni muda mrefu pengine kuliko hata urefu wenyewe. Kwa nini Simba hii tena inayopewa nguvu na Mohammed Dewji ‘MO’ inashindwa kutamba mbele ya Yanga? Ni swali ambalo mashabiki wengi wa Simba hawana majibu.

Yaani katika kipindi ambacho Simba imekuwa ikipata shida mbele ya Yanga, huko Kimataifa imekwenda robo fainali mara mbili. Yaani Simba inafungwa na Yanga hapa lakini inawafunga Al Ahly. Ni ajabu na kweli. Lakini ukweli ambao haujasemwa ni Yanga imefanikiwa kutawala Dabi ya Kariakoo baada ya uwekezaji wa Gharib Said Mohammed ‘GSM’.

Ni wazi mwekezaji huyu mpya ameweka nguvu katika masuala kadhaa ikiwemo kuhakikisha timu hiyo inashinda mechi ya Dabi.

Hii ndiyo nguvu ya Yanga kwa sasa. Wachezaji wamekuwa wakiingia katika Dabi na ahadi kubwa ya bonasi endapo watashinda mchezo huo. Hii imekuwepo kwa miaka hii mitatu sasa. Wachezaji wa Yanga wanafahamu wakishinda tu, wanavuta mpunga mrefu.

Unajua kwa nini GSM ameamua kuweka nguvu kubwa zaidi katika Dabi? Nitakupa sababu mbili halafu wewe utaangalia ipi ina mashiko zaidi.

Sababu ya kwanza, ni kuweza kushinda mioyo ya Wananchi kirahisi. Yanga ilikuwa imekaa muda mrefu bila kushinda taji lololote. Na GSM alifahamu wazi kushinda taji itahitaji muda zaidi, lakini njia pekee ya kuanza kuwafurahisha Wananchi ni kuanza kutawala Dabi.

Kabla ya GSM Yanga ilikuwa ikionewa sana katika mechi hizi za Dabi ya Kariakoo, lakini ujio wake ukalimaliza hilo ndani ya muda mfupi tu.

Sababu ya pili, GSM anafanya biashara ya jezi za Yanga. Anahitaji biashara yake iwe kubwa na kuuzika zaidi. Unawezaje kuuza jezi zaidi? Ni kuifanya Yanga iwe timu nzuri zaidi. Katika kuboresha hilo, aliona fursa ya kufanya biashara zaidi kupitia hizi Dabi.

Leo hii mashabiki wa Yanga wanaona fahari kuvaa jezi mpya na kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao katika Dabi ya Kariakoo kutokana na matokeo mazuri waliyopata hivi karibuni. GSM amefanikiwa kuunganisha Dabi na biashara ya jezi. Ni mkakati mzuri.

Sababu ya mwisho ni Simba kuanza kuichukulia Dabi ya Kariakoo kama mchezo mwingine wa kawaida. Kutokana na nguvu kubwa wanayoweka katika mashindano ya kimataifa, Simba ni kama imeanza kuichukulia poa mechi hii ya Dabi.

SOMA NA HII  BALAA LAZIDI KUMUANDAMA CHAMA...ZAMBIA NAKO WAMFUNGIA VIOO...MOSES PHIRI NAYE HAYUMO ETI......