Home Habari za michezo HAWA CLUB AFRICAIN WAPINZANI WA YANGA CAF…KIKOSI CHA TU NI ZAIDI YA...

HAWA CLUB AFRICAIN WAPINZANI WA YANGA CAF…KIKOSI CHA TU NI ZAIDI YA BIL 21…

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga watakwenda kucheza mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutinga hatua ya makundi dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Kwa mujibu wa droo iliyopangwa wiki iliyopita jijini Cairo, Misri yalipo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Yanga itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 2, kabla ya kwenda Tunisia kumalizia mechi ya mkondo wa pili itakayopigwa Novemba 9, mwaka huu.

Yanga itacheza na timu hiyo, baada ya kusukumizwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoka sare nchini kwenye mechi ya kwanza na kufungwa bao 1-0 mchezo wa marudiano.

Club Africain inakumbukwa vema msimu huu kwa kuiondosha timu ya Tanzania, Kipanga ya Zanzibar kwa mabao 7-0 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ni timu kongwe ambayo mashabiki wengi wa kizazi cha sasa hawaijui vizuri, lakini kwenye miaka ya 1980 hadi 1990 ilikuwa moja kati ya timu tishio nchini Tunisia na barani Afrika, hapa tunaimulika kwa undani zaidi…

Timu ya tatu kwa ubora Tunisia

Kwa sasa inatajwa kama ni timu ya tatu kwa ubora nchini humo baada ya Esperance na Etoile du Sahel ambazo ndizo zinazotamba nchini Tunisia kwa sasa na kupata nafasi za kuiwakilisha nchi hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Club Africain na CS Sfaxien zikipaswa kukita kambi kwenye Kombe la Shirikisho.

Bingwa wa Afrika mwaka 1991

Ilitwaa ubingwa wa Afrika mara moja, ambapo mwaka 1991 ikiuchukulia kwenye Uwanja wa Nakivubo, Kampala nchini Uganda.

Ilifanikiwa kuingia fainali na kucheza dhidi ya SC Villa, ambapo kwenye mechi ya kwanza nchini Tunisia, Uwanja wa El Menzah ilitoa kipigo cha mabao 6-2 Novemba 23, na kwenye mechi ya marudiano timu hizo zikatoka sare ya bao 1-1 nchini Uganda, Desemba 14, 1991, Club Africain ikakabidhiwa kombe lake nchini humo kwa ushindi wa jumla ya mabao 7-3.

Fainali Shirikisho 2011

Mafanikio mengine makubwa ya timu hiyo ni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika 2011 dhidi ya Maghreb de Fes ya Morocco na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 6-5.

Ikiwa nyumbani Novemba 19, mwaka huu, ilishinda bao 1-0, lakini ikaenda kupoteza kwa idadi kama hiyo nchini Morocco, Desemba 4, hivyo timu hizo zikalazimika kuingia kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti na ndipo ilipolikosa kombe hilo.

Makundi Ligi ya Mabingwa mara moja

Club Africain imefanikiwa kuingia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja tu. Nayo ilikuwa ni msimu wa 2018/19 na haikufanikiwa kabisa kutinga hatua ya robo fainali, yaani kushika nafasi mbili za juu.

Ikiwa kwenye Kundi C, timu hiyo ilishika nafasi ya tatu ikimaliza na pointi 10 sawa na CS Costantine ya Algeria, lakini ikizidiwa mabao ya kufunga, hivyo wenzao wakashika nafasi ya pili na kwenda robo fainali, TP Mazembe akiliongoza kundi kwa pointi 11, Ismailia ya Misri ikishika mkia kwa pointi mbili.

Makundi mara tatu Kombe la Shirikisho

Timu hiyo inawania kuingia kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya nne. Imeshafanya hivyo mara tatu, kuanzia 2008, 2011 ilivyokwenda mpaka hatua ya fainali na 2017 ilipoingia na kuishia hatua ya nusu fainali ilichapwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Super Sport United ya Afrika Kusini, baada ya kutoka sare nyumbani bao 1-1, kabla ya kwenda kufa nchini Afrika Kusini kwa mabao 3-1.

Kikosi cha bilioni 21 za Kibongo

Club Africain imepitia kipindi kigumu kwa siku za karibuni kutokana na kuyumba kiuchumi, na kama haitoshi kuwa adhabu ya kutoruhusiwa kusajili wachezaji katika madirisha matatu.

Hii ilitokana na kushindwa kumlipa Mchezaji Mghana Nicholas Opoku baada ya kuvunja naye mkataba. Hali hiyo ya ukata ilisababisha kuondokewa na nyota wao kadhaa akiwamo kinara wa mabao msimu uliopita, Yassine Chamack aliyejiunga Al Ahly Tripoli ya Libya.

Hata hivyo, kwa sasa wanaonekana kujipanga kwani ina kikosi chenye thamani ya Dola za Marekani milioni 9.29 zaidi ya Sh. bilioni 21 za Tanzania.

SOMA NA HII  NI WIKIENDI YA KIBABE YENYE MECHI KALI ZA KUBASHIRI NA MERIDIANBET....