Home CAF YANGA vs CLUB AFRICAIN:…FANYEENI YOOTEE LAKINI HILI LA MWAMUZI MKILISAHAU IMEKULA KWENU….

YANGA vs CLUB AFRICAIN:…FANYEENI YOOTEE LAKINI HILI LA MWAMUZI MKILISAHAU IMEKULA KWENU….

Hakuna lugha yoyote ambayo mashabiki, wanachama wa Yanga na Watanzania wanataka kusikia leo saa 10 jioni kwenye mechi dhidi ya Club Africain zaidi ya ushindi mnono ndani ya Uwanja wa Mkapa.

Hilo ndiyo pekee linaloweza kuiweka Yanga kwenye nafasi nzuri ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho na kupooza machungu ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika wiki chache zilizopita.

Wachezaji na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said wamesisitiza wamejiandaa kikamilifu kumaliza mchezo huo nyumbani kwani tayari wanajua changamoto za ugenini na matakwa ya mashabiki kwa heshima ya klabu.

Kinachowapa Yanga jeuri kujua udhaifu wa wapinzani wao kimbinu, kiufundi na kimazingira ambao wamepanga kuutumia vyema kupata ushindi mnono leo kwani hata jana mtoto wa Nabi, Hedi Nabi aliucheza mchezo huo kimbinu.

MABADILIKO NA KIKOSI

Yanga ilinasa mpango wa Club Africain kuwepo nchini kuitazama kwenye baadhi ya mechi na baada ya kugundua hilo, benchi la ufundi chini ya Nasreddine Nabi wakapumzisha mastaa muhimu kwenye mechi za KMC na Geita Gold. Jambo ambalo linaweza kuwashangaza wageni wao leo.

Uamuzi wa kuomba mechi hiyo kuchezwa saa 10:00 ni miongoni mwa akili kubwa iliyofanywa na Yanga ili kunufaika na udhaifu wa wapinzani wao kukabiliana na hali ya joto ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu Club Africain.

Udhaifu wa Club Africain kiufundi ni makosa ya walinzi wao wa pembeni kuachia mianya mara kwa mara kwa kupenda kushambulia na Yanga imepanga kuitumia kupata mabao mengi kwa haraka.

Mawinga wa Yanga watabeba jukumu kubwa la kuhakikisha timu yao inapata ushindi mnono leo kwani wao ndio wanaotegemewa kutumia udhaifu huo wa walinzi wa pembeni wa Club Africain kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Hapa ndipo Yanga wanapaswa kuwa na uchaguzi sahihi wa wachezaji wa kucheza nafasi husika ili waweze kuvuruga muundo wa kiulinzi wa Club Africain.

Kasi, maamuzi ya haraka pindi wawapo na mpira mguuni, uwezo wa kupiga pasi za mwisho na hata kufunga wa Farid Musa na Bernard Morrison unaweza kuwa silaha muhimu kwa Yanga leo iwapo wawili hao wataanzishwa katika winga ya kulia na kushoto.

Mbali na hilo, nidhamu ya hali ya juu inahitajika kwa walinzi wa pembeni wa Yanga katika kuwadhibiti mawinga wa Club Africain hasa katika upigaji wa mipira ya krosi ambayo imekuwa ikitumiwa vyema na washambuliaji wao katika kufunga mabao.

Pia upande wa kiungo, Yanga inapaswa kuhakikisha haiwapi nafasi viungo wa Club Africain kulisogelea lango lao mara kwa mara kutokana na uwezo wao mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali. Hivyo Yanga huenda ikaanza hivi;

Langoni huenda akaanza kipa Diarra Djigui kama kawaida, kulia Djuma Shaban, kushoto Kibwana Shomari huku Yannick Bangala na Dickson Job wakicheza kama mabeki wa kati.

Katika kiungo Khalid Aucho na Feisal Salum wanapewa nafasi kubwa ya kuanza kama viungo wa chini wawili huku Feisal akiwa na jukumu la kuongeza idadi katika mashambulizi sambamba na mawinga wawili wa pembeni ambao ni Jesus Moloko na Bernard Morrison.

Kule mbele Fiston Mayele atasaidiana na Stephaine Aziz KI katika kusaka mabao.

UTAMU WA HISTORIA

Historia ya miaka michache iliyopita pamoja na matokeo ya wapinzani wao mara ya mwisho pindi walipotua kwenye ardhi ya Tanzania, yanawapa jeuri na matumaini Yanga kuibuka na ushindi muhimu dhidi ya Club Africain kwenye mechi hiyo.

Yanga imewahi kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili ambazo ni 2016 na 2018 na ilifuzu katika hali kama ya sasa na ilitolewa katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa na kuangukia katika hatua ya mchujo ya mwisho ya mashindano hayo na kuzitoa Sagrada Esperanca ya Angola na Welayta Dicha ya Ethiopia katika nyakati hizo mbili tofauti. Mashabiki wa Yanga na wadau wa soka nchini wanaweza kupata hofu kutokana na historia ya kutofanya vizuri katika uwanja wa nyumbani pindi inaposhiriki mashindano ya klabu Afrika lakini matokeo ya Club Africain ugenini yanaweza kuwajengea hali ya kujiamini kutokana pia na wapinzani wao hao kutokuwa mwiba ugenini. Kuthibitisha hilo, katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Yanga imecheza nyumbani, imepata ushindi mara tatu, kutoka sare nne na kupoteza tatu kama ilivyo kwa Club Africain ambayo katika mechi zao 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika wameshinda tatu, sare nne na kupoteza tatu.

REFA WA FILIMBI

Kumbukumbu za mwamuzi Celso Armindo Alvacao kutoka Angola atakayechezesha mechi hiyo, hapana shaka zinawalazimisha Yanga na benchi lake la ufundi kuhakikisha nidhamu ya hali ya juu kutokana na hulka yake ya kupenda kumwaga kadi.

Refa huyo katika michezo 21 ya kimataifa aliyochezesha kabla ya mchezo wa leo, amegawa kadi 83 ikiwa ni wastani wa kadi 3.9 kwa kila mchezo na kati ya hizo, kadi 81 ni za njano huku kadi nyekundu zikiwa ni mbili.

Alvacao atasaidiwa na Waangola wenzake ambao ni refa msaidizi namba moja Venestancio Tomas Cossa na Teofilo Paulo Mungoiwakati refa wa akiba akiwa ni Wilson Julio Muiange.

Katika mechi hizo 21 zilizochezeshwa na refa huyo mwenye umri wa miaka 33, timu zilizokuwa nyumbani zimeshinda mara tisa, za ugenini zimeshinda mara sita na jumla ya mechi sita zilimalizika kwa matokeo ya sare.

WAKUCHUNGWA

“Skander Laabidi ni beki wa kulia jasiri, anajiamini ingawa hali ya kujiamini sana kuna wakati amekuwa akijikuta anasababisha hatari langoni kwake, aliwahi kulaumiwa kwa makosa hayo mara kadhaa katika mechi za ligi ya Tunisia.

“Nader Ghandri ni beki mwingine bora kwenye mipira ya vichwa akiwa na nguvu na akili iliyotulia. Taoufik Cherifi ndiye kiungo wao bora wa ukabaji, kuna wakati pia hutumika kama beki wa kati, ana ubora wa kujenga mashambulizi lakini akiwa na ubora wa kupokonya mipira,” alisema Hedi Nabi ambaye ni mtoto wa Kocha wa Yanga, Nabi Mohammed.

“Abdenour Belhoucini ni winga wao jasiri anayejua kukimbia kwa hesabu nzuri na kutoa pasi zenye athari. Kuna mwingine anaitwa Zouhaier Dhaouadi ni kiungo mshambuliaji wa nyuma ya mshambuliaji wa mwisho mwenye uzoefu mkubwa kuliko mwingine.”

DAKIKA ZA MOTO

Yanga inapaswa kuingia na mpango mzuri wa mchezo wa kujichunga zaidi na dakika 30 za mwisho, pia kutumia udhaifu wa wapinzani wao kuwamaliza.

Club Africain ni timu ambayo imekuwa ikifunguka mara kwa mara na kucheza kwa kushambulia katika dakika 30 za mwisho jambo ambalo limekuwa likiifanya ipate idadi kubwa ya mabao katika muda huo lakini kinyume chake ndio muda ambao hujikuta ikiruhusu idadi kubwa ya mabao hasa inapokutana na wapinzani walio vizuri katika kushambulia kwa kushtukiza.

Kati ya mabao 21 ambayo Club Africain imefunga katika mechi 20 zilizopita, mabao 11 imepachika katika dakika 30 za mwisho na kati ya mabao 13 iliyofunmgwa, mabao saba ni katika muda huo.

SOMA NA HII  'KUDADEKI' HII SIMBA YA HUKU MISRI NI SUKARI NA ASALI TUPU AISEE.....'MASTA' MAKI ATAMBULISHA MIFUMO 3 YA KUIUA YANGA...