Yanga imepokea taarifa njema baada ya mshambuliaji wake, Yacouba Sogne kutamka hadharani kwamba sasa yuko sawa kurejea kazini ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Akizungumza Yacouba alisema baada ya kukaa nje kwa msimu mzima na nusu akiuguza majeraha ya goti lake kisha kupewa matibabu ya kisasa, sasa yuko tayari kurejea kazini kuitumikia timu hiyo.
Novemba 2,2021 Yacouba aliumia katika dakika ya 31 wakati Yanga ikicheza dhidi ya Ruvu Shooting kisha kulazimika kukaa nje kwa msimu mmoja na nusu akiuguza majeraha ambapo Yanga ililazimika kumpeleka nchini Tunisia kwa matibabu.
Yacouba alisema kwasasa yuko sawa na kwamba anasubiri maamuzi ya mabosi wa klabu yake juu ya kurejea kundini kufuatia kuondolewa katika usajili wa msimu huu.
“Kwa sasa niko sawa kabisa namshukuru Mungu nimekuwa katika matibabu, nitarejea uwanjani kucheza wakati wowote,”alisema Yacouba.
“Nawashukuru mashabiki wote, viongozi na madaktari ambao walisimamia matibabu yangu, mashabiki wasubiri muda si mrefu wataniona tena uwanjani.
Daktari huyu hapa
Daktari aliyesimamia matibabu ya mshambuliaji huyo, Youssef Mohamed alisema kwa sasa raia huyo wa Burkina Faso yuko sawasawa baada ya kupona vizuri na hata kufanya mazoezi ya kutosha.
Youssef alisema walikuwa katika mapambano makubwa kusimamia matibabu ya mshambuliaji huyo kutokana na bado alikuwa ni mchezaji mwenye ubora mkubwa kurejea tena uwanjani.
“Hii hatua ambayo amebakiza sasa ni mambo ya kiutawala lakini Yacouba alishapona muda mrefu na alichokuwa anafanya ni kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili,”alisema Youssef raia wa Tunisia.
“Tuliamini kwamba ni mchezaji ambaye kwa umri wake bado anaweza kuja kuwa na mchango mkubwa na hata majeraha yake yaliluwa yanatibika, niwashukuru sana viongozi wa Yanga na wadhamini wetu, GSM kwa jinsi walivyopambana naye, hii ilikuwa ni hatua ya ukomavu wao mkubwa.”