WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikitimiza raundi ya 13, winga wa Azam FC, Ayoub Lyanga ndiye anayeongoza kwa kutoa pasi nyingi za mabao akiwa na ‘assist’ sita huku kipa wa Simba, Aishi Manula ndiye mlinda mlango mwenye ‘cleen sheet’ nyingi, imefahamika.
Manula ambaye juzi aliruhusu bao moja katika sare ya goli 101, ana jumla ya ‘clean sheets’ nane mpaka sasa.
Kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu, mchezaji anayeshika nafasi ya pili kwa kutoa pasi nyingi zilizozaa mabao ni Sixtus Sabilo kutoka Mbeya City ambaye pia anakamata nafasi ya pili kwenye ufungaji bora akiwa na mabao saba chini ya Fiston Mayele anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji bora kwa mabao yake nane kibindoni.
Sabilo ana ‘assist’ tano mpaka sasa, na wanaoshika nafasi ya tatu ni Clatous Chama, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ wote wa Simba na Saido Ntibazonkiza wa Geita Gold ambao wote wao wametoa pasi za mwisho nne.
Kwa upande wa makipa, Manula amecheza mechi nane mpaka sasa bila kuruhusu wavu wake kuguswa, akifuatiwa na Ali Ahmada wa Azam FC akiwa na ‘clean sheets’ sita, huku Mcomoro mwenzake Mahamoud Mroivili wa Coastal Union akiwa na tano.
Makipa ambao wana ‘clean sheets’ nne mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ni Djigui Diarra wa Yanga, Jonathan Nahimana wa Namungo, Metacha Mnata wa Singida Big Stars, na Said Kipao wa Kagera Sugar.