Home Habari za michezo KISA KUSOTA SANA BENCHI…MWAMNYETO AVUNJA UKIMYA YANGA…AFUNGUKA NABI ‘ALIVYOMTRITI’….

KISA KUSOTA SANA BENCHI…MWAMNYETO AVUNJA UKIMYA YANGA…AFUNGUKA NABI ‘ALIVYOMTRITI’….

Habari za Yanga

Kikosi cha Yanga mchana wa jana kiliwasili kwenye Mji wa Tunis kikitokea Sousse, nchini Tunisia huku ikishuhudiwa mubashara na nahodha wake, Bakar Nondo Mwamnyeto akitamba kuwa, wale wanaochonga dhidi yake na timu hiyo kwa ujumla wajiandae kupata sapraizi ya aina yake.

Yanga ipo Tunisia kwa ajili ya kuwahi pambano la marudiano la play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kuitinga makundi, mechi itakayopigwa keshokutwa mjini Tunis, baada katika mechi ya awali, kulazimishwa suluhu Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mechi hiyo ijayo, Yanga inahitaji sare ya mabao au kushinda ili kurejea rekodi ya kutinga makundi ya Shirikisho mwaka 2016 na 2018 kupitia hatua hiyo ya play-off, huku nahodha huyo, akifunguka wachezaji wapo tayari kufanya kile kinachosubiriwa na Watanzania.

Akizungumza Mwamnyeto alisema wamekaa na benchi la ufundi pamoja na viongozi kuhakikisha wanafanya kilicho bora na wao kama wachezaji wanafanya kila namna kuhakikisha wanapata matokeo huku akikiri kuwa kikosi kipo tayari na wanatambua umuhimu wa mchezo huo.

“Tuna dakika 90 ngumu, subirini muone, kwani kama wachezaji tumejiandaa na tumejipanga kufanya kilicho bora. Ni mchezo muhimu kwa kila upande kila mmoja amejiandaa, hivyo atakayefanya vizuri ndiye atakayesonga hatua inayofuata kwa upande wa viongozi, benchi la ufundi wamemaliza mambo yote kazi imebaki kwetu,” alisema Mwamnyeto na kuongeza;

“Tunaomba ushirikiano kutoka kwa Watanzania wenye mapenzi na timu yetu nafasi tunayo, ni suala la muda tu kila kitu kinawezekana kama wao waliweza kutuzuia nyumbani sisi tunashindwa vipi kuwazuia kwao.”

Ishu yake iko hivi

Nahodha huyo pia, alifunguka wakati anaopitia ndani ya kikosi hicho, lakini akisema bado ana uwezo wa kufanya vizuri, japo anahitaji kuaminiwa zaidi ili kuendeleza ubora wake alionao kuanzia misimu miwili iliyopita na akikiri akipewa muda atafanya kilicho bora.

“Nimeanza vibaya msimu huu, sina nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti kama ilivyokuwa misimu iliyopita, hiyo inaweza kuwa sababu ya kuwa na makosa madogo madogo kwani napoteza kujiamini lakini uwezo wa kucheza bado ninao,” alisema Mwamnyeto na kuongeza;

“Hakuna mchezaji anayependa kucheza dakika chache uwanjani nina imani na kipaji changu, nitapewa muda wa kucheza kukosea kusinifanye nikaonekana sina ninachokifanya. Nikikosea kesho nipewe tena ili kurekebisha makosa kitendo cha kunikalisha benchi kinanipa mzigo mkubwa wa kuamini sina ninachokifanya ni mbaya kwangu.”

AFICHUA SIRI NA NABI

“Nimekaa na kocha ameniambia, mimi ni mchezaji mzuri na ni mfano wa kuigwa ndani ya timu, hivyo nikiyumba nitaipoteza timu, kwa hiyo natakiwa kutuliza akili na kusawazisha makosa ili kuirudisha timu kwenye mstari hasa eneo la ulinzi ambalo amekiri kuwa limekuwa na makosa mengi msimu huu,” alisema beki huyo aliyewahi kutamba na Coastal Union na kuongeza;

“Kocha kaniambia nikae niangalie michezo yangu niliyopata kuicheza ili nijue wapi pa kuanzia na kusawazisha kile ambacho nimebaini kuwa hakikuwa sawa ndani ya muda niliocheza hilo nimelifanyia kazi nitarudi uwanjani na kuendelea pale nilipoishia nahitaji kuwa bora na kuwa mfano kwa wengine.”

Yanga jana ikijifua katika uwanja wa mazoezi uliopo ndani ya Hoteli ya Elmouradi iliyopo Mji wa Sousse ikitumia saa mbili za nguvu kuhakikisha wanakuwa bora katika ulinzi na kuhakikisha makosa ya ukabaji hayatokei na kujipanga kucheza krosi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUSIKIA SIMBA WATASHUSHA 'FULL KIKOSI'...KOCHA KAGERA SUGAR AGUNA KISHA AFUNGUKA HAYA...