Home Geita Gold FC MPOLE: GEITA WANANIONEA…MBONA WENGINE HAWAKO NA TIMU NA WANALIPWA MSHAHARA…

MPOLE: GEITA WANANIONEA…MBONA WENGINE HAWAKO NA TIMU NA WANALIPWA MSHAHARA…

Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, George Mpole, ameibuka na kufunguka mengi makubwa yanayomuhusu mara baada ya kutoonekana kwa muda kikosini hapo.

Hiyo ikiwa siku ni siku chache zimepita tangu uongozi utoe taarifa za mshambuliaji huyo kutoweka kambini wakati timu hiyo ikiendelea kucheza michezo ya Ligi Kuu Bara.

Mpole alisema hayupo katika timu hiyo, kutokana na kuuguza majeraha ambayo hivi sasa yanaendelea vizuri baada ya kutumia gharama zake mwenyewe.

Mpole alisema anawashukuru wale ambao wanajali uwezo wake, hasa Watanzania wanaompenda na kuona umuhimu wake kwa kumpigia simu wakimtakia heri akiwa anaendelea kujiuguza.

Aliongeza kuwa anashangazwa na uongozi wake kugomea kumlipa mshahara wake, kwa sababu ya kutokuwa na timu wakiwa wanafahamu kabisa yeye ni majeruhi na daktari ana taarifa zake.

“Viongozi wanaosema Mpole hayupo kwenye timu ndio haohao waliosema nisiwekewe mshahara kwa sababu sitaki kucheza, wakati kiuhalisia mimi nina majeraha.

“Mimi sijalipwa mshahara na timu ambayo nimepata majeraha nikiwa naipambania ili ipate matokeo ugenini, sijalipwa mshahara kwa sababu zisizo za msingi, daktari wa timu taarifa zangu anazo. Kuna wachezaji wengine wapo nyumbani zaidi ya miezi miwili na wanalipwa, lakini mimi nimeumia siku chache siwekewi mshahara.

“Lakini nashukuru kwa sasa naendelea vizuri, watu wananipa ushirikiano na tayari nimeanza mazoezi, muda si mrefu nitarudi,” alisema Mpole.

Wakati Mpole akiyasema hayo, uongozi wa Geita Gold umeibuka na kukanusha vikali tuhuma hizo kutoka kwa mshambuliaji wao.

Mkuu wa Idara ya Habari wa Geita Gold, Hemed Kivuyo, alisema: “Uongozi haukuwa na taarifa zozote kuhusiana na Mpole kuwa na majeraha.

“Nakumbuka tulipokuwa Tanga kucheza dhidi ya Coastal Union, baada ya mchezo huo Mpole aliomba ruhusa ya kwenda Dar, akasema ataungana na timu kuelekea mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting ambao ulifanyika jijini Dar.

“Kweli tulivyofika Dar aliungana na timu mazoezini, lakini kwa muongozo wa Kocha Mkuu (Fred Felix Minziro) alisema atatumia wachezaji ambao walicheza kwenye mechi iliyopita dhidi ya Namungo.

“George Mpole ni mchezaji wetu na kikubwa anachotakiwa kufanya ni kuzungumza na uongozi ili kumaliza tofauti au sintofahamu inayoendelea na hatimaye arejee ndani ya timu.”

Mara ya mwisho Mpole kuonekana uwanjani ilikuwa Oktoba 13, mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Geita Gold na Coastal Union zilishindwa kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  YANGA YA ENG HERSI NA GSM YAZIDI KUTAKATA CAF....SIMBA MHHHH....!!!