Home Habari za michezo KICHAPO CHA YANGA CHAIBUA MAPYA IHEFU…YALIYOFANYIKA NYUMA YA PAZIA HAYA HAPA…

KICHAPO CHA YANGA CHAIBUA MAPYA IHEFU…YALIYOFANYIKA NYUMA YA PAZIA HAYA HAPA…

Habari za Yanga

Gumzo kubwa wiki hii ni Yanga kufungwa kwa mara ya kwanza kwenye ligi baada ya mechi 49 mfululizo na kumaliza rasmi ubabe wa ‘unbeaten’ yao iliyodumu tangu Aprili 25, mwaka jana ilipofungwa na Azam bao 1-0.

Stori za kupoteza kwa Yanga kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya zimekuwa nyingi kutokana na kufungwa na Ihefu mabao 2-1, tena Ihefu iliyopanda daraja, ikitokea nyuma na kupata ushindi.

Kwenye huzuni hii ya Yanga kumekuwa na mengine mengi nyuma ambayo yanafariji au kubadili mwelekeo kwa wengine bila kujua.

Yawezekana kukawa na mengi ambayo yametokea tangu Yanga ilipopoteza mchezo huo ambayo yameonekana na mengine hayaonekani, yafuatayo ni baadhi ya vilivyobadilika au kujitokeza baada ya Yanga kufungwa.

WASAHAU MACHUNGU

Miongoni mwa timu zilizopitia wakati mgumu tangu kuanza kwa msimu huu ni Ihefu ambayo tangu ligi ianze imekuwa ikipambana kuhakikisha inatoka mkiani na mambo yamekuwa magumu kwao.

Ushindi dhidi ya Yanga umewafanya kuandikisha ushindi wa tatu msimu huu na angalau kufikisha pointi 11 baada ya mechi 14, ikiwa imefungwa mechi tisa na sare mbili pekee.

Lakini kwa vyovyote hali waliyonayo sasa Ihefu hata machungu waliyopitia miezi michache iliyopita yamepoa na wanajisikia faraja mno kumfunga bingwa mtetezi asiyefungika na kinara wa ligi.

Kingine hata Ihefu wenyewe hii ndiyo mara yao ya kwanza wanaifunga Yanga tangu walipoanza kukutana nayo msimu wa 2020-21 kabla ya kushuka mwisho wa msimu na kupanda tena msimu huu.

Yanga imekutana na Ihefu kwenye ligi mara mbili kabla na kuifunga mabao 3-0 kisha kuibamiza mabao 2-0. Kwa kifupi Ihefu haikuwahi kuifunga hata kutikisa nyavu za Yanga mpaka ilipovunja mwiko huo kwa nguvu zote.

TIMU ZAFURAHIA

Kufungwa kwa Yanga kumezifanya timu kama Simba na zingine kufurahia, kwani mbabe wao amepata mwamba, ambaye ni Ihefu. Kupoteza kwa Yanga kumefanya sasa walingane na Azam kwa pointi wakiwa na tofauti ya mechi moja pekee.

Hiyo imeihamasisha Azam iendelee kukaza buti kwa kuwa mpinzani wao aliyekuwa hatabiriki atapunguza lini kasi tayari amekubali kushikwa shati na sasa mbio zimekuwa na unafuu angalau.

Lazima Azam ipate nguvu kwa kuwa nayo imepambana kushinda mechi zake saba mfululizo zilizopita hivyo morali ya ushindi waliyonayo na anguko la Yanga kwao inakuwa hesabu iliyokamilika,kazi kwao sasa.

Kipekee pia wapinzani na mahasimu wakubwa wa Yanga, Simba wamefurahi mno. Kwanza kwa mpinzani kufungwa, pili tambo na kejeli zipungue mtaani, tatu pengo la pointi baina yao limepungua pia.

Ni ukweli usiofichika kwamba Simba pamoja na kupambana kushinda mechi zake lakini ushindi mfululizo wa Yanga ulikuwa ukiwavuruga mno kwani ilikuwa ikiwaweka mbali na ndoto za kutwaa ubingwa msimu huu.

Msimu uliopita, Simba iliukosa ubingwa ambao wameutwaa mara nne mfululizo kabla ya sasa kutetewa na Yanga na safari hii waliamini wanaweza kuupigania tena ubingwa huo lakini kasi ya Yanga ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwao kuliko ilivyokuwa ikifikiriwa.

YANGA MCHEZONI

Kipigo hiki inawezekana kimewarejesha Yanga kwenye soka la ushindani wa kweli, ufundi na mbinu za kutosha kuhakikisha wanapata pointi tatu kila mchezo.

Soka huwa linaamuliwa na kipaji, juhudi, mbinu na bahati pia. Nachelea kusema ni kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikiongozwa na bahati kuliko hivyo vingine nilivyovitaja hapo juu.

Ndiyo, kwenye soka hiki ni kitu cha kawaida kokote duniani kuiona timu inashinda hata kwenye mchezo ambao iliaminika wangeweza kufungwa, sasa Yanga wameishi na hilo jambo muda mrefu sasa.

Inafika wakati mnaingia uwanjani, mwili wote unaamini ushindi kabla ya mapambano na unahisi ushindi ndiyo halali yako, sasa pengine kwa kushtushwa usingizini sasa Yanga itarejea vizuri kimbinu, mikakati na ushindani zaidi.

KITENDAWILI YANGA

Kwa haraka haraka timu ya mwisho kukaa muda mrefu bila kufungwa utaitaja Azam ambayo ilitwaa ubingwa wa 2013-14 bila ya kupoteza mchezo hata mmoja katika mechi 38 za ligi wakati huo.

Baada ya hapo utaitaja Yanga na mechi zao 49, idadi hii si ndogo na wala si ya kubeza. Yanga imefanya kitu kikubwa kutengeneza rekodi hii ambayo pengine itachukua muda mrefu mno kuvunjwa.

Na hata atakayeivunja anapaswa kutumia nguvu kubwa kufika hapo kwani ushindani unazidi kuongezeka na mpira unazidi kuwa mgumu kila kukicha, hivyo Yanga ya Mtunisia, Nasreddine Nabi itaendelea kukumbukwa kwa rekodi hii nzito na ngumu.

LIGI YAANZA UPYA

Kufungwa kwa Yanga, ligi imetabasamu sasa, sidhani kama kuna timu kati ya 15 zilizobaki ambayo haijafurahia anguko hilo la Yanga.

Kila timu ilikuwa haifui dafu, itafungwa tu au itatoa sare kwa kutegemea au pasipo kutegemea, timu nyingine zote zilikuwa zinalia kasoro Yanga tu ndiyo iliyokuwa ikicheka au kukaa kimya lakini sio kununa kisa imefungwa.

Ni wazi Ihefu imekuwa mtetezi wa timu nyingine na sasa zimefurahi baada ya kilio na huzuni waliyokuwa nayo kabla na baada ya kukutana na Yanga kwa maana ya kutambua ni ngumu kuwafunga vijana hao wa Jangwani.

Sasa ligi inaanza upya, hakuna mwoga tena kabla ya mechi na Yanga zaidi ya wasiwasi wa ugumu wa mechi. Hakuna tena mbabe wa wenzake wote 15 waliobaki na hakuna ambaye hajafungwa tangu kuanza kwa msimu.

Ihefu imezifanya timu na wengine waamini hakuna kinachoshindikana chini ya jua na kwamba lolote linawezekana ukijipanga kwa ajili ya kutafuta unachokitaka hata kama ni kigumu kiasi gani.

SOMA NA HII  BAADA YA KUPIGA MPIRA PAPATUPAPATU SIMBA WAOMBA UTULIVU SASA