Home Habari za michezo PAMOJA NA BARBARA KUTIMKA SIMBA….HAYA HAPA MAMBO MAZITO ALIYOYAFANYA KWA MIAKA MIWILI...

PAMOJA NA BARBARA KUTIMKA SIMBA….HAYA HAPA MAMBO MAZITO ALIYOYAFANYA KWA MIAKA MIWILI TU…..

Habari za Michezo

Septemba 5, 2020 Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ilimteua Barbara Gonzalez kuwa CEO mpya wa klabu hiyo akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Senzo Mazingiza Mbatta ambaye alitimkia Yanga. Kuteuliwa kwake kulileta maneno miongoni mwa wadau wa soka wakihoji uwezo wake hasa kwenye masuala ya soka na ukaribu wake kikazi na mwekezaji Mo Dewji.

Taarifa ya Simba kuhusu uteuzi wake ikazima maneno yote kwani iliweka wazi nafasi mbalimbali alizopitia ndani ya klabu hiyo na uzoefu wake wa uongozi wa soka japo alikuwa nyuma ya pazia. Baada ya hapo kilichofuata ni utendaji kazi wake ambao kiuhalisia ameitendea haki nafasi hiyo na kukidhi matarajio ya mashabiki na wanachama wa Simba.

Chini yake, Simba imeshinda ubingwa wa ligi, Kombe la ASFC, imefika Robo Fainali Klabu Bingwa Afrika, Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho na anaiacha Simba ikiwa kwenye hatua ya makundi Klabu Bingwa Afrika. Kwenye upande wa uchumi ambao ndiyo sehemu hasa aliyobobea, Simba imefanikiwa kupata mikataba mikubwa ikiwemo kampuni ya M-bet (Tsh bilioni 26.1), mkataba na Vunjabei (Tsh bilioni 2), mkataba na Africarriers, ATCL na mingine midogo midogo.

Kwenye uongozi wake pia Simba imeendelea kukua zaidi kupitia mitandano ya kijamii kutokana na kuwekeza nguvu na teknolojia ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa Simba App na jambo kubwa zaidi ni mipango ya hatua ya pili ya uendelezaji wa ujenzi katika uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju, ambao kwa sasa upo katika hatua ya kuzungusha ukuta.

Kilichowashtua wengi ni uamuzi wake wa kujiuzulu kwenye kipindi hiki ambacho klabu inaelekea kwenye mzunguko wa pili wa ligi na michuano ya Klabu Bingwa Afrika, maswali ni je, ni kweli anaondoka kutokana na sababu alizozieleza au kuna jingine kubwa ambalo lipo ndani ya uongozi?. Kuondoka kwake kunamaanisha nini kwa mwekezaji Mohammed Dewji ambaye ndiye alimuamini kwenye nafasi hiyo tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi?

Maswali haya hayana majibu mpaka pale ambapo mwekezaji Mohamed Dewji atatoa neno lake kwa mashabiki na wanachama wa Simba ambao wanazidi kujiuliza kuhusu hatma ya klabu yao huko mbeleni ambako ndiyo kugumu zaidi kuliko hivi sasa.

SOMA NA HII  BALEKE ATAMBA KWENYE ANGA ZA WABABE HAWA WA YANGA