Home Habari za michezo UKIONA YANGA WANACHEZA JUMANNE TU…NENDA KABET WANAFUNGWA…TAKWIMU HIZI HAPA…

UKIONA YANGA WANACHEZA JUMANNE TU…NENDA KABET WANAFUNGWA…TAKWIMU HIZI HAPA…

Kikosi cha Yanga SC

Hadithi tamu kwa jezi nyeusi kwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga na namna ilivyoibeba timu hiyo kabla ya kuwekewa zengwe na kwenda kupasuka kwa Ihefu 2-1, ilivuma sana masikioni mwa wapenda soka.

Baada ya kupasuka kwa Ihefu na kutibuliwa rekodi ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza ikikwamisha ya 49, iliporudi kwenye mechi mbili zilizofuata ikivaa jezi hizo na kushinda dhidi ya Tanzania Prisons na Namungo, yaani kwa taarifa yako tu, Yanga haijawahi kupoteza mchezo ikiwa imetinga uzi huo mweusi.

Lakini ukiachana na bahati na jezi hizo nyeusi, mabingwa hao wa kihistoria wana rekodi ya kusisimua ya mechi za Jumanne. Yanga imekuwa na bahati mbaya na siku hiyo, kwani rekodi zinaonyesha imekuwa ikipasuka kila ikitia mguu uwanjani kwenye mechi za siku hizo ukiacha mechi chache.

LIGI KUU

Katika mechi za Ligi Kuu Bara imetoboa mara chache sana ikicheza Jumanne, kwani hata kipigo kilichotibua rekodi ya kucheza michezo 50 bila kupoteza, ilitibuliwa siku hiyo na Ihefu pale Uwanja wa Highland, Mbarali jijini Mbeya.

Mechi hiyo ilipigwa siku ya Jumanne Novemba 29 ikiwa mkononi na mechi 49 tangu ilipopoteza kwa Azam Aprili 25, 2021, ikilingana na Arsenal ya England iliyoweka rekodi hiyo hadi ilipofungwa na Man United na vijana wa Jangwani wakanyooshwa 2-1 na Ihefu. Siku hiyo pia Yanga haikuvaa jezi nyeusi.

Pia, rekodi zinaonyesha tangu Ligi ya Bara iasisiwe mwaka 1965, Simba na Yanga zimekutana mara mbili tu siku ya Jumanne, ikiwamo pambano la kihistoria ambalo Yanga ilipasuliwa mabao 6-0 na watani wao hao na kushindwa kujibu mapigo hadi leo hii.

Kama hujui mechi hii ilipigwa Jumanne ya Julai 19, 1977 ambapo ndipo iliandikwa ‘hat trick’ ya kwanza ya ya pekee kwenye mechi ya watani, ikiwekwa na King Abdallah Kibadeni.

Mechi ya mwisho ya dabi kupigwa Jumanne ilikuwa ni ile ya Oktoba 27, 1992 na kwa mara nyingine tena Yanga ikalala mbele ya Simba kwa kufungwa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Damian Kimti, lakini hata kwenye Dabi ya Mzizima, Yanga imeshanyooshwa na Azam mechi iliyopigwa Mei 28, 2019 kwa kulazwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Daniel Amoah na Mudathir Yahya.

HUKO CAF NAKO

Hata kwenye mechi za kimataifa, Yanga imekumbana na bahati mbaya ya siku hiyo ya Jumanne, kwani Machi 6, 2018 ilipasuka 2-1 kwa Township Rollers ya Botswana katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika enzi hizo timu hiyo ikifundishwa na Mzambia George Lwandamina.

Licha ya Obrey Chirwa anayekipiga kwa sasa Ihefu kuisawazishia Yanga baada ya Rollers kutangulia kupitia kwa Lemponye Tshireletso na dakika hya 83 Motsholetsi Sikele akatupia la pili na hata zilipoenda kurudiana Machi 17 mwaka huo ziliishia kutoka suluhu na Yanga kutolewa michuanoni.

Juni 28, 2016 ilishuka tena uwanjani Jumanne katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo na Yanga ikachapwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Merveille Bokadi, likiwa pambano la hatua ya makundi ya michuano hiyo na ilipoenda kurudiana tena ikapigwa 3-1.

Mechi hiyo ya marudiano ilipigwa tena Jumanne, ila ilikuwa ni Agosti 23, 2016 na Yanga kuzamishwa kwa mabao ya Jonathan Bolingi na Rainford Kalaba aliyefunga mawili huku bao la kufutia machozi la vijana wa Jangwani likiwekwa kimiani na Amissi Tambwe, huku beki Andrew Vincent ‘Dante’ akilimwa kadi nyekundu dakika ya 30 tu.

Yanga ilikumbana na kipigo kingine cha mechi hizo za makundi siku ya Jumanne ya Julai 26, 2016 iliponyolewa 3-1 na Medeama ya Ghana kwa mabao ya Daniel Amoah kabla hajasajiliwa Azam, na Abbas Mohammed aliyefunga mawili na bao la kufutia machozi liliwekwa na Simon Msuva kwa tuta.

Katika kundi hilo, Yanga ikicheza kwa mara ya kwanza hatua hiyo kwa Kombe la Shirikisho Afrika ilimaliza nafasi ya nne ikiburuza mkia mbele ya Mazembe, MO Bejaia ya Algeria na Medeama, kama ilivyokuwa mwaka 2018 ilipocheza tena hatua hiyo ikiwa ni rekodi kwao na timu za Tanzania enzi hizo.

Aliyekuwa Kocha wa Mbeya City na Tanzania Prisons na Polisi Morogoro, Mohamed ‘Adolf’ Rishard alisema suala la kufungwa Yanga siku ya Jumanne kwake anaamini ni matokeo ya kawaida tu ya mchezo wa mpira wa miguu na hayana uhusiano wowote.

“Hivi karibuni kulikuwa na suala la wao wakivaa eti jezi nyeusi wanashinda sasa hizo zinabaki imani ingawa kwangu naamini siku waliyofungwa wamecheza vibaya na wanaposhinda basi wamecheza vizuri kama timu,” alisema.

Nyota wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila alisema sio rahisi watu kulizingatia ila anachokiamini michezo waliyocheza siku hiyo walikutana na wapinzani waliojiandaa vizuri kuliko wao.

SOMA NA HII  RASMI...CHIKO USHINDI MALI YA YANGA...UONGOZI TP MAZEMBE WAFUNGUKA MAKUBALIANO YOTE ...