Home Habari za michezo KISA CAF…NABI NA MGUNDA WAINGIA KWENYE MTIFUANO NA TFF…HOJA ZAO HIZI HAPA…

KISA CAF…NABI NA MGUNDA WAINGIA KWENYE MTIFUANO NA TFF…HOJA ZAO HIZI HAPA…

Kocha wa Simba, Juma Mgunda ambaye timu yake inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na yule wa Yanga ambao wanacheza Kombe la Shirikisho, Nasreddine Nabi wameungana kulalamikia ratiba ya michuano ya kimataifa.

Simba na Yanga wanaanzia ugenini kukabiliana na vigogo wenzao kwenye makundi waliyopangwa wakipishana tarehe, Simba ikianza Februari 10 dhidi ya Horoya ya Guinea huku Yanga wakikipiga Februari 12 na US Monastir ya Tunisia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti makocha wa timu hizo walisema kuwa wasiwasi wao ni mechi zilivyokaribiana na za ligi ambazo zimekuwa zikiwaongezea uchovu mkubwa sambamba na majeruhi ambao wamekuwa wakiongezeka.

“Wakati wa kuamua ubora wetu zaidi katika mechi hizi sita ni sasa. Unaona jinsi ratiba ya mechi hizi za ligi zilivyo karibu lakini kitu kinanitesa zaidi ni majeruhi ambao wamekuwa wakiongezeka kwa sasa.

“Haya yote tunatakiwa tuyafanyie tathimini sasa tuamue juu ya maisha yetu ya sasa na baadaye. Tukifanikisha hili sioni ugumu kwa Yanga kutoa ushindani bora kulingana na malengo yetu. Siyo kundi rahisi ni kundi ambalo linatulazimu kuwa na mipango sahihi,” alisema Nabi.

Alisema hata hivyo, Yanga haina cha kuhofia na kwamba kama watajipanga vyema kabla ya mechi hizo Februari 12, 2023 watapambana nao.

“Kila timu ina ubora wake sioni kama ni rahisi kusema tupo katika kundi rahisi, nafikiri hata wao watalazimika kutuheshimu kwa kuwa tuko nao pamoja.”

Kwa upande wa Mgunda, alisema matumizi ya mastaa wake yatakuwa makubwa na wachezaji wakicheza mechi mfululizo ni rahisi kupata majeraha hivyo wanatarajia ugumu japo mashindano yamewapa fursa kujipanga.

Mgunda ambaye amekiri kuwa ligi msimu huu ni ngumu kutokana na kushindwa kufikia malengo yake ndani ya mzunguko wa kwanza, ameliambia Mwanaspoti kuwa Simba na Yanga zitakuwa na wakati mgumu mzunguko wa pili.

Alisema ratiba ya ligi itawapa mwanya wa maandalizi kuelekea mashindano hayo, lakini pia itachangia kwa kiasi kikubwa kuwachosha wachezaji ambao wanahitaji nguvu zaidi ili kwenda kufanya vyema kwenye mashindano hayo.

“Mechi ni bandika bandua, upana wa kikosi hauwezi ukawa chachu kwa sababu kuna aina ya wachezaji ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.”

Simba katika Ligi ya Mabingwa imepangwa kundi C na Raja Casablanca, Horoya na Vipers, ilhali Yanga katika Kombe la Shirikisho imepangwa kundi D ikikutana na TP Mazembe, US Monastir na Real Bamako.

SOMA NA HII  WACHEZAJI TP MAZEMBE WAKATWA MISHAHARA...KWA KUSHINDWA KUVUKA MAKUNDI