Home Habari za michezo SIMBA SC, YANGA SC NA AZAM FC NI MTAFUTE MTAFUTE…MMOJA LAZIMA ALIE...

SIMBA SC, YANGA SC NA AZAM FC NI MTAFUTE MTAFUTE…MMOJA LAZIMA ALIE KESHO…

Habari za Yanga

Kikosi cha Simba kipo Mwanza kikitokea Bukoba kilipokwenda kumalizana na Kagera Sugar, tayari kwa mechi yao ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, huku wakani zao Yanga wakiwa bado Dar es Salaam kujiandaa kubanana na Azam FC iliyokuwa Mjini Geita.

Timu hizo zinazochuana kwenye msimamo wa ligi zikiwa ndani ya Tatu Bora zitarudi uwanjani tena baada ya kumaliza kazi ya raundi ya 17, huku kila moja ikiwa na kibarua cha kuzimaliza dakika 180 za jasho na damu za kufungia mwaka 2022.

Yanga inaoongoza msimamo imezidi kujikita kileleni baada ya majuzi kuifumua Coastal Union mabao 3-0, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 ugenini na Geita Gold na Simba yenyewe juzi usiku ilivaana na Kagera Sugar na kutoka sare ya 1-1, ikiwa ni sare ya kwanza kwa timu hizo katika mechi 17 zilizopita baina ya timu hizo.

Baada ya mechi hizo, timu hizo kuanzia wikiendi hii, zitakuwa bize kuanza kupambana kwenye dakika 180 ili kumaliza mwaka 2022 kibabe.

Tuanze na Yanga na Azam. Timu hizo zitakuwa kwenye pambano la pamoja na kutiana ubaya wakati zitakaposhuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na kumbukumbu ya sare ya mabao 2-2, iliyopatikana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Septemba 6. Mchezo huu utakuwa ni wa 30 kwa timu hizi kukutana tangu Azam FC ilipopanda rasmi Ligi Kuu Bara 2008, ambapo kati ya hiyo Yanga imeshinda mechi 11, sare tisa na kupoteza tisa.

Timu hizi zimekuwa na ushindani mkali pindi zinapokutana kwani Yanga imefunga mabao 35 na Azam imefunga 33.

Mara ya mwisho kwa Azam kuifunga Yanga ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0 Aprili 25, 2021 kisha kucheza michezo 49 bila ya kupoteza tangu ilipokuja kufungwa 2-1 na Ihefu Novemba 29.

Yanga itafunga mwaka kwa kusafiri hadi Manungu Complex kucheza na Mtibwa Sugar Desemba 31, ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza mabao 3-0, Septemba 13 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mtibwa Sugar haina rekodi nzuri inapocheza na Yanga kwani kwenye michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara imefungwa yote huku ikiruhusu jumla ya mabao manane bila ya wao kufunga hata moja.

Mchezo wa mwisho kwa Mtibwa Sugar kuifunga Yanga ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0 ilioupata Aprili 17, 2019.

Kwa upande wa Simba baada ya kumalizana na Kagera juzi, itajiandaa kushuka uwanjani siku ya Boxing Day, itakapokuwa jijini Mwanza kuumana na KMC.

Timu hizo zinakutana jijini humo baada ya wenyeji KMC kuomba mchezo huo upigwe huko, huku kukiwa na kumbukumbu ya mechi ya awali baina yao kumalizika kwa sare ya 2-2 zilipoumana Septemba 7.

Tangu KMC imepanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19, imekutana na Simba mara tisa na katika hizo zote haijashinda ikifungwa jumla ya michezo minane na kutoka sare mmoja tu.

Katika michezo hiyo yote Simba imefunga jumla ya mabao 20 wakati kwa upande wa KMC wao imefunga sita tu.

Simba itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa Desemba 30, kucheza na Maafande wa Tanzania Prisons ikiwa na kumbukumbu ya kushinda bao 1-0, mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Septemba 14.

Ushindi mkubwa kwa Simba dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni wa mabao 5-0, Februari 28, 2015.

Azam baada ya kubanwa na Geita juzi na kisha kuvaana na Yanga siku ya Krismasi, itarudi tena uwanjani Desemba 31, siku ya kuuaga rasmi mwaka 2022 kwa kuumana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa raundi ya kwanza kwa bao 1-0 Septemba 13.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex baina ya timu hizi zilifungana mabao 2-2 Desemba 18, 2021.

Timu yoyote itakayochanga vyema karata zake kwenye mechi hizo mbili za kufungia mwaka 2022, zitazifanya ziingie 2023 kibabe wakati zikipanda meli kwenda visiwani Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi inayoanza rasmi Januari Mosi na kufikia tamati Januari 13.

Simba ndio watetezi wa Mapinduzi, imepangwa Kundi C la michuano hiyo, wakati Yanga ipo Kundi B na Azam wapo Kundi A sambamba na timu nyingine mbilimbili na kama zitaongoza makundi hayo zitafuzu nusu fainali kama itakavyokuwa kwa timu za Kundi D, lenye Namungo, Chipukizi na Aigle Noir ya Burundi.

KAULI ZA MAKOCHA

KOCHA Mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema ushindani umekuwa mkali hususani ugenini, hivyo jukumu lao ni kuandaa kikosi chao kukabiliana na mazingira ya aina yoyote.

Kocha wa Azam FC, Kally Ongala alisema bila jitihada za makusudi ni ngumu sana kupata matokeo mazuri kwani kila mpinzani naye amejipanga pia vizuri.

Kocha Nasreddine Nabi wa Yanga alisema ligi ila bado alikiri ushindani kuongezeka ukichagizwa zaidi na mrundikano wa ratiba unaoendelea kuwakabili.

SOMA NA HII  DODOMA JIJI HAWAPOI WALA HAWABOI....WAENDELEA KUSHUSHA MAJEMBE YA NGUVU...SIMBA NA YANGA ZIJIANGALIE...