SIMBA SC imeendelea kupunguza Pointi dhidi ya Vinara Yanga SC baada ya kupata ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba SC walianza kupata bao dakika ya 12 likifungwa na John Bocco ,akimalizia pasi ya Kiungo fundi Saidi Ntibazonkiza na katika dakika ya 24 Prisons walipata pigo baada ya Samson Mbangula kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mlinzi wa Simba SC,Henock Inonga.
Licha ya kupata pigo hilo Prisons walisawazisha bao kupitia kwa Mshambuliaji wao Jeremia Juma dakika ya 30 hadi mapumziko timu hizo zilienda zikiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili Simba SC walipata bao la mapema dakika ya 46 likifungwa na yule yule John Bocco kwa kazi nzuri ya Pape Ousmane Sakho na dakika ya 60 Saidi Ntibazonkiza alipigilia msumari wa tatu akimalizia kazi ya Clatous Chama.
