Kiungo wa Yanga SC, Zanzibar Heroes na Taifa Stars Feisal Salum Abdallah amekwea pipa leo kuelekea Ulaya kupitia Falme za Kiarabu, akiacha timu yake inamenyana na Mtibwa Sugar mchezo wa Ligi Kuu.
Feisal ambaye yupo kwenye mgogoro wa Kimkataba na klabu yake ya Yanga SC baada ya yeye kuvunja Mkataba kwa kutumia vipengele vya mkataba huo na kujitangaza kuwa huru.
Alhamisi wiki hii aliibukia viwanja vya Mao Tse Tung nyumbani kwao Zanzibar ambako alionekana akicheza mazoezi na klabu ya JKU ambayo ilimuibua kiungo huyo nyota nchini.
Yanga SC walitoa taarifa rasmi ya klabu wakisema kiungo huyo ni mchezaji na mali yao mpaka 2024 kama mkataba unavyosema na kwamba yeye amekiuka vipengele vya Mkataba baina yao.
Kumekuwa na maneno meengi juu ya wapi alipo mchezaji huyo baada ya kuvunja mkataba na Yanga SC Alhamisi ya tarehe 22.12.2022 na nani yuko nyuma yake.
Wadau wengi wa Yanga SC walisema kijana amerejea kambini Avic Town na kwamba jambo limekamilika, viongozi wengi wamejinasibu kuongea nae na kusema wamemaliza tatizo lakini kijana bado anaonekana kushikilia msimamo wake wa kuachana na Yanga.
Baada ya taarifa nyingi mitandaoni kuihusisha klabu ya Azam FC kuwa inamrubuni mchezaji huyo, klabu hiyo ilikanusha kupitia Mtendaji Mkuu wake kwamba haihusiki na lolote.
Leo Feisal katika post yake ya Instagram amesema amefika kuanza majukumu yake mapya. Hali hii inaonyesha kwamba kuna timu nje ya nchi pia inahitaji huduma ya kiungo huyo za Kizanzibar aliyekuwa anaitumikia Yanga SC.
Nini kinafuata baada ya hapa na nini itakuwa hatima ya jambo hili ambalo limechukuwa mgogoro wa Kimkataba ni jambo la kusubiri na kuona, kwani mkataba ni makubaliano ya kisheria.