Home Habari za michezo MGUNDA:- HIZI GOLI TANO TANO…TUTAWAPIGA SANA WANAOKUJA KIZEMBE MBELE YETU…

MGUNDA:- HIZI GOLI TANO TANO…TUTAWAPIGA SANA WANAOKUJA KIZEMBE MBELE YETU…

Kocha Msaidizi Simba, Juma Mgunda

Baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold kwenye mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu, katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza juzi, Klabu ya Simba imetamba kuendeleza dozi nene kwa timu zingine huku Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda, akiwashukuru na kuwasifu wachezaji wake kwa kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mgunda alisema wachezaji wa timu yake kwa siku za karibuni wamekuwa wakicheza kwa kupambana na kutaka kufanya vema, pamoja na uchu wa kufunga mabao kitu ambacho kinampa faraja.

“Nilisema hakuna mechi rahisi, haijalishi matokeo, tulijipanga vizuri kucheza mechi ngumu kwa sababu Geita Gold ni timu nzuri na mwalimu wake Minziro (Fred Felix) ni kocha mzuri na mshindani tangu anacheza soka, kwa hiyo hata anavyofundisha soka anafundisha lile la kushindana. Soka ni mchezo wa nafasi, mkipata nafasi na kuzitumia vema basi inakuwa siku nzuri kwenu, Geita Gold wamefanya makosa mengi tumewaadhibu.

“Nawashukuru wachezaji wangu, wanaonekana kadri muda unavyozidi kwenda wanazidi kubadilika, inanipa moyo wa kupambana kutaka kufanya vizuri na kutaka kufunga magoli unaonekana ni mkubwa sana,” alisema Mgunda.

Mchezaji Kibu Denis ambaye juzi alifunga bao lake la kwanza msimu huu, alisema anaamini atakuwa na mwendelezo mzuri kwenye ufungaji baada ya kufungua akaunti.

“Ulikuwa mchezo mgumu, mechi haikuwa rahisi, binafsi nimetokea benchi na kufunga bao, nishukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi, wanachama na mashabiki wa Simba ni kweli nilipofunga bao nilifurahi sana kwa sababu ndiyo bao langu la kwanza msimu huu, ukiangalia msimu uliopita nilifunga mabao manane, mashabiki walitegemea makubwa msimu huu kutoka kwangu, lakini hawakuyaona mzunguko wa kwanza. Kila kitu kina muda wake, nimeanza kwa kufunga bao leo, naamini huu ni mwanzo mzuri kuelekea mechi zinazofuata,” alisema.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kipigo hicho ni ujumbe tosha kwa timu zingine zote, huku akitoa onyo kuwa vipigo vinene kama hivyo vitaendelea.

“Hii ni kutoa ujumbe kuwa sisi tuna timu bora sana, kutoa kipigo cha mabao 5-0 tena timu ikiwa ugenini haijawahi kutokea kwenye Ligi Kuu msimu huu na sisi ndiyo tuna rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye ligi, tulishinda pia kwa idadi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar, kuna watu walimbeza Clatous Chama kuelekea kwenye mechi hii, lakini amewafunga midomo, amefunga bao zuri sana, unajua wakati Argentina inajivunia fundi wa mpira, Messi (Lionel), sisi Simba tunajivunia mtu anaitwa Chama,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here