Katika kitu ambacho Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameishukuru Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wiki hii, ni uamuzi wa kumsogezea mbele siku mbili mechi dhidi ya Ruvu Shooting.
Nabi amesema uamuzi huo umeongeza chachu ya kuimarika kwa kikosi ambacho amekiri kuwa kilikuwa na ‘fatiki’ na sasa hata mastaa wapya wataingia.
Yanga ni mwenyeji leo Jumatatu usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na mechi ya kwanza walishinda 2-1.
Akizungumza Nabi alisema kurejea kwa wachezaji wote kambini ni chachu ya maandalizi bora na ya ushindani wakihakikisha wanacheza kwa mafanikio mzunguko wa pili ambao ni maalumu kumalizia ligi na kutetea ubingwa.
“Kikosi kipo kamili na tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka fiti kuelekea mchezo na Ruvu Shooting ambao umesogezwa mbele hadi Jumatatu (leo), ni furaha kwangu kwani imesaidia kuwaweka wachezaji kwenye utimamu kutokana na kuwa kwenye fatiki,” alisema.
“Ongezeko la siku mbili limeongeza chachu ya kuimarisha kikosi na naamini wachezaji wangu watakuwa kwenye ubora na wataingia wakiwa timamu. Natarajia matokeo mazuri kutoka kwao pamoja na changamoto ya ushindani itakayokuwepo.”
Nabi alisema wanahitaji kumaliza mzunguko wa pili kwa kukusanya pointi kila mchezo ingawa wanatambua haiwezi kuwa rahisi, lakini wamejiandaa.
Yanga inaongoza msimamo ikiwa imekusanya pointi 53 baada ya kucheza mechi 20 inakutana na Ruvu Shooting ambayo imecheza michezo 20 na pia imekusanya pointi 14 ikiwa katika nafasi ya 15 kwenye msimamo.
Kikosi hicho cha Jangwani kikimalizana na Ruvu kitacheza na Namungo kabla ya kuhamia kwenye makundi ya Shirikisho Afrika watakapozivaa Monasir na TP Mazembe kwenye mechi mbili mfululizo.