Home Habari za michezo LICHA YA GOLI LA KANOUTE ‘KUUA MTU’ JANA….HIZI HAPA DONDOO MUHIMU ZA...

LICHA YA GOLI LA KANOUTE ‘KUUA MTU’ JANA….HIZI HAPA DONDOO MUHIMU ZA AJABU KATI YA SIMBA vs COASTAL..

Simba vs coastal union

BAO la Sadio Kanoute katika dakika ya 56 limetosha kuipeleka Simba katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), huku wana fainali wa msimu uliopita, Coastal Union wakiaga rasmi michuano hiyo.

Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huo wa hatua ya 32 bora uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba ilifika hatua hii baada ya kuifunga Eagle FC mabao 8-0 huku Coastal Union ikiifunga Tanga Middle 3-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Mwaka 1967 ndio ambao michuano hii iliasisiwa, ingawa wakati huo ilikuwa ikifahamika kama mashindano ya Kombe la FAT.
Ilipofika mwaka 2002 ilikuwa ni mara ya mwisho kuchezwa kwa Kombe la FAT kwani baada ya hapo michuano hiyo ilishindwa kuendelea na ilisimama kwa takriban miaka 13 mfululizo.

Baada ya kusimama ilipofika mwaka 2015 ilirejeshwa upya na kubadilishwa jina kuitwa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) likiwa ni jina ambalo linaendelea kutumika hadi leo kutokana na udhamini uliowekwa na Azam.

Tangu michuano hii imeanza kuchezwa mwaka 1967, ikifahamika Kombe la FAT na sasa ASFC, Yanga ndio timu pekee iliyobeba taji mara nyingi zaidi ya timu nyngine ikifanya hivyo mara sita katika miaka ya 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016 na 2021-2022.

Inayofuata baada ya Yanga kubeba taji hilo mara nyingi ni Simba ambayo imelibeba mara nne miaka ya 1995, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021 wakati Mtibwa Sugar na Tanzania Stars zikichukua mara mbili kila mmoja.

Simba imelipa kisasi kwa Coastal Union kwani ilishawahi kuondolewa hatua ya robo fainali ya ASFC baada ya kufungwa kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika msimu wa 2015/2016.

Msimu uliopita Coastal Union ilifika fainali na kupoteza mbele ya Yanga kwa penalti 4-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Julai 2, mwaka jana. Awali timu hizo zilifungana mabao 3-3 ndani ya dakika 120.

Ushindi huu unaifanya Simba kusonga mbele na sasa itakutana na African Sports huku michezo ya 16 bora ikitarajiwa kupigwa kati ya Machi 3 hadi 5 mwaka huu.

SOMA NA HII  SIMBA YATOA TAMKO KUHUSU HATMA YA MORRISON