Home Habari za michezo UCHAGUZI MKUU SIMBA:..MWANACHAMA 1000 TU KUPIGA KURA LEO…MAMBO YA KUZINGATIA HAYA HAPA…

UCHAGUZI MKUU SIMBA:..MWANACHAMA 1000 TU KUPIGA KURA LEO…MAMBO YA KUZINGATIA HAYA HAPA…

Mkutano Mkuu Simba

WANACHAMA, wapenzi na mashabiki wa klabu ya Simba wanahesabu dakika kabla ya kushuhudia klabu hiyo ikifanya Uchaguzi Mkuu kupata viongozi wapya watakaoiongoza kwa miaka mingine minne ijayo.

Wagombea 14 wanachuana kwenye uchaguzi huo utakaofanyika leo Jumapili jijini Dar es Salaam utakaochagua mwenyekiti mpya na wajumbe watano kuingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo iliyopo kwenye mchakato wa kuendeshwa kwa hisa.

Kwa takribani wiki mbili wagombea walikuwa wakinadi sera katika kampeni zilizofunguliwa Januari 16, ili kuwashawishi wanachama watakawaopigia kura kuwachagua leo na kampeni hizo zilifungwa usiku wa leo kabla ya  asubuhi hii  kuamkia ukumbini kusubuiri uamuzi wa wapiga kura.

Katika kipindi hicho wanachama wamesikia sera za wagombea, wakiwamo wawili wanaowania nafasi ya uenyekiti na 12 ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka upande wa wanachama ambao wataungana na wale wa upande wa mwekezaji anayetambuliwa kwa sasa – Mohammed Dewji.

Kilichobaki baada ya kampeni hizo ni uamuzi uliyopo mikononi mwa wanachama kuchagua wanayemtaka miongoni mwa wagombea.

Nafasi inayotolewa macho zaidi ni ile ya mwenyekiti inayowaniwa na wagombea wawili, baada ya wengine kuenguliwa kwa kukosa vigezo na sifa za kushiriki akiwamo makamu mwenyekiti na makamu wa rais wa zamani wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.

Waliopitishwa kwenye nafasi hiyo na ambao wamekuwa wakichuana kumwaga sera kwa wanachama ni anayetetea kiti, Murtaza Mangungu na Moses Kaluwa.

Kaluwa anagombea kwa mara ya kwanza, huku akionekana kumpa upinzani mkali Mangungu aliyechaguliwa mwaka juzi katika uchaguzi mdogo ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Swedy Nkwabi aliyejiuzulu miezi kama saba tu tangu alipochaguliwa 2018.

Wagombea wengine wa uchaguzi huo ambao awali ulionekana kukosa msisimko kabla hya mambo kubadilika ni wale wanaowania ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ambao ni Dk Seif Ramadhan, Seleman Haroub, Idd Kitete na Issa Idd.

Wengine ni Abubakari Zebo, Abdallah Mgomba, Elisony Mweladzi, Rashid Mashaka, Rodney Makamba, Aziz Mohamed, Asha Baraka na Pendo Mapugilo.

Mgawanyiko

Kipindi chote cha kampeni za uchaguzi kimewagawa katika makundi mawili wanachama wa klabu hiyo. Kuna wanaomuunga mkono Mangungu anayetetea kiti na wengine kwa Kaluwa.

Awali, uchaguzi huo ulionekana kama umepoa vile, lakini ndani kwa ndani kulikuwa na mchuano mkali kwa wagombea, ingawa yote katika yote wenye uamuzi wa kuwasimika madarakani kuongoza miaka minne ijayo ni wanachama.

Sio mikoa yote imefikiwa na wagombea hao, bali baadhi yao walitumia vyombo vya habari kuongea na wanachama kuwaomba kura zao.

Isikie kamati

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Boniface Lihamwike amekuwa akisisitiza na kuwataka wagombea kufanya kampeni za amani, akiwasihi waachane na chuki kwani italeta mpasuko kwa wanachama baada ya uchaguzi.

“Lengo la uchaguzi ni kupata viongozi bora watakaoleta maendeleo ya Simba, hivyo hakuna haja za wagombea kufanya kampeni zisizo na nidhamu. Kikubwa kila mmoja amepewa nafasi ya kunadi sera zake na wenye uamuzi wa mwisho wa kumchagua wanayemtaka ni wanachama,” anasema Lihamwike.

Mwenyekiti huyo anamtaka kila mgombea kwa nafasi yake na wanachama lazima ajue yapo maisha mengine baada ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kutunza utu na thamani ya mwingine.

“Pamoja na presha nyingi za uchaguzi zisivuke mipaka. Maana baada ya hapo tutakutana sehemu moja kwa ajili ya kutoa sapoti kwa Simba. Wengine kazini, mtaani na kwingineko, hivyo kila mtu lazima azingatie utu wa mwingine,” anasema.

Anasema wanachama hai hadi sasa wako 1,000 ambao wanatoa ada kila mwezi na ndio wenye sifa ya kuchagua viongozi wapya katika uchaguzi utakaofanyika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Posta, katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Utaratibu

Kuhusu utaratibu kwenye uchaguzi huo utakaoanza asubuhi, Lihamwike anasema: “Wanachama watatakiwa kufika mapema na kuorodhesha majina, kwani kabla ya uchaguzi kutakuwa na Mkutano Mkuu wa wanachama ambao hautakuwa chini yangu na ukimalizika ndipo tutajua uchaguzi unaanza saa ngapi ambao nao nitausimamia mimi.”

Mwenyekiti huyo anaamini kila kitu kitakwenda sawa na matokeo yatatangazwa mapema ili mambo mengine yaendelee. Miongoni mwa waangalizi na waalikwa kwenye uchaguzi huo ni maofisa kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wabunge ambao ni wanachama wa klabu hiyo iliyoasisiwa 1936.

Uongozi

313 Siku alizodumu Swedy Nkwabi kama Mwenyekiti Simba kati ya Nov 5, 2018 hadi Sept 14, 2019.

Feb 7, 2021 ndio siku Mangungu alipochaguliwa mwenyekiti katika uchaguzi mdogo leo ni siku 719.

Jan 29 Tarehe ya uchaguzi mkuu wa Simba utakaofanyika Ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.

14 Idadi ya wagombea wote waliopitishwa kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu.

SOMA NA HII  KAMATA SLOT YA BURSTING HOST UJIMWAGE NA MAMILIONI YA CASINO ZA MERIDIANBET...